Habari za Kitaifa

Mvua, joto na baridi zitazidi katika maeneo haya

Na  BENSON MATHEKA December 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya  imewatahadharisha Wakenya kujiandaa kwa mvua  mara  kwa mara  hadi Jumanne, Desemba 24.

Katika ushauri wake, idara ya utabiri wa hali ya hewa ilitangaza kuwa Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa la Kati na Kusini, Nyanda za Juu Kusini Mashariki na Pwani zitapata mvua.

Kaunti za Nyanda za Juu Mashariki za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi na Nairobi zinatarajiwa kupata mvua ya wastani hadi kubwa katika muda wa siku tano kuanzia Jumamosi Desemba 21.

Kulingana na  idara hiyo utabiri umeonyesha kuwa kaunti za Nyanda za Juu Mashariki zitapata mvua  kiasi  asubuhi lakini itanyesha sana mchana.

Kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet na Nandi zinatarajiwa kupokea mvua zaidi ya wastani katika kipindi cha siku tano zijazo.

Mvua katika kaunti zilizotajwa hapo juu ilitarajiwa hasa alasiri na itaambatana na radi huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikiwataka wakazi kuwa macho dhidi ya mafuriko ambayo yanaweza kutokea.

Kaunti zingine ambazo zilitarajiwa kukumbwa na hali sawa ya anga ni pamoja na Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Kaunti ya Pokot Magharibi.

Kaunti za pwani za Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale pamoja na sehemu za pwani za Kaunti ya Tana River zilitarajiwa kupata mvua ndogo asubuhi na alasiri.

Huku maeneo kadhaa nchini yakitarajiwa kukumbwa na mvua wikendi hii, idara ya utabiri wa hali ya anga pia iliwatahadharisha wakazi wa Kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi kuhusu majira ya baridi kali usiku.

Kulingana na idara hiyo, kaunti hizo zilitarajiwa kukumbwa na baridi kali kwa siku tano zijazo. Halijoto ya usiku inatarajiwa kushuka hadi nyusi 11°C.

Vile vile, viwango vya juu vya joto mchana vinatarajiwa katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet na Kakamega.

Halijoto  mchana katika maeneo haya inatarajiwa kuzidi nyusi 30°C huku kaunti za pwani za Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale zikitabiriwa kukumbwa na kiwango sawa cha joto.