• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Benki ya Dunia yamwaga mamilioni Nakuru kufadhili kilimo

Benki ya Dunia yamwaga mamilioni Nakuru kufadhili kilimo

NA RICHARD MAOSI

Wakulima Kaunti ya Nakuru Jumanne walipokezwa kitita cha Sh9.5 milioni na Benki ya Dunia ili kuanzisha miradi ya kujiendeleza kimaisha.

Walikongamana katika eneo la Soilo mjini Nakuru, ambapo walijadili maswala muhimu yakiwemo teknolojia, uhaba wa chakula na njia za kukabiliana na hali mbaya ya anga msimu wa kiangazi.

Wakulima waliolengwa ni kutoka mashinani, katika hafla ya mradi wa National Agricultural and Rural inclusive Development Growth Project (NARIGP).

Kaunti ndogo za Bahati, Molo, Naivasha, Njoro na Kuresoi Kaskazini ziliwakilishwa ,ambapo wakulima wengi ni wafugaji wa kuku, nyuki, ng’ombe na viazi.

Waziri wa kilimo Kaunti ya Nakuru Bi Immaculate Maina akiwahutubia wakulima. Picha/ Richard Maosi

Wadi 14 kati ya 20 zinazopatikana mjini Nakuru zitafaidika na mradi wenyewe ambao, ulibuni makundi nane ya washiriki waliofuzu kupata ufadhili wenyewe baada ya kupitia mchujo.

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Naibu gavana Dkt Erick Korir,Waziri wa Kilimo Bi Immaculate Maina Njuthe na afisa mkuu wa kilimo Bw Joel Kibet.

Dkt Korir aliwataka wakulima kuwekeza katika kilimo biashara ili kujiongezea mapato, kwa kutafuta soko la nje ambalo halina mazao yanayotoka kaunti ya Nakuru.

Aidha walitakiwa kujianzishia miradi mbadala mbali na ufugaji,ambayo ingesaidia kaunti kukua kiuchumi hasa wakati huu,ambapo kaunti ya Nakuru inakaribia kupata hadhi ya kuwa jiji.

Hela hizo pia zitawasaidia wamiliki wa matrakta ya kulima. Picha/ Richard Maosi

“Kaunti ya Nakuru itakuwa ni kielelezo bora kwa kaunti nyinginezo nchini zinazolenga kujikita kikamilifu katika miradi ya kuwainua wakulima wadogo wasiokuwa na mtaji wa kutosha,”akasema.

Korir alishukuru serikali kuu kwa kuteua kaunti ya Nakuru kama mojawapo ya maeneo yatakayofaidika na mradi wa NARIGP unaoendeshwa katika kaunti 20.

Milioni 9.5 ni asilimia 40 ya fedha zilizotengewa mradi wenyewe ambapo asilimia 60 zilizosalia zitatolewa kwa hatua,kulingana na matumizi ya wakulima.

Alisema kuwa afisi ya gavana inatambua mchango wa kilimo katika ukuaji wa uchumi wa kaunti ya Nakuru, katika juhudi za kupigana na umaskini na kubuni nafasi nyingi za ajira.

Miradi ya ufugaji nyuki sasa imepigwa jeki. Picha/ Richard Maosi

Kwa upande mwingine Bi Immaculate Maina alisema kaunti ilipokea mapendekezo 125 kutoka kwa wakulima, wakitafuta ufadhili wa benki ya dunia lakini ni 55 tu waliofanikiwa.

Aliongezea kuwa shughuli yenyewe iliendeshwa kwa uwazi na usawa bila mapendeleo ,na waliobahatika kufaidika walikuwa wanastahili.

“Ninajivunia kuwa mshikadau atakayefanikisha mradi wa kilimo katika kaunti ya Nakuru kwa hisani ya benki ya dunia,”Immaculate alisema.

Aliongezea kuwa mnamo 2018 kaunti ya Nakuru iliongoza kwa kutoa lita milioni 250 ya maziwa katika soko la kitaifa hii ikiwa ni rekodi ya kupigiwa mfano.

Wakulima waliohudhuria kutoka kaunti ndogo nane za Nakuru wakinuia kupata ufadhili. Picha/ Richard Maosi

Wakulima walishauriwa kutumia uwazi ,hasa ijapo katika swala la kufanyia makadirio ya fedha kufanyia miradi ya kujiendeleza.

Pia Nakuru ni kaunti nambari mbili nchini kuzalisha viazi ambapo huzalisha tani 12 katika kila ekari ,na mwaka huu huenda wakulima wakapata mazao zaidi,kwa kuonyesha ari ya kujizidishia kipato.

Ushirikiano baina ya wizara ya kilimo na wakulima wadogo umehakikisha kuwa hawakosi mbolea,mbegu,ushauri nasaha wa bure na mifumo mbalimbali ya kiteknolojia kufanyia kilimo.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali mkulima Stanley Kiproro kutoka Kuresoi South,kiongozi wa jamii ya Ogiek alisemahuu ni mwamko mpya kwa jamii za wafugaji ambao bado wanaishi msituni.

Akiwa muuzaji wa asali anasema kikundi anachowakilisha kilitengewa milioni 1.7,ili kuwekeza katia mradi wa kufuga nyuki.

Ufugaji kuku sasa utapigiwa upatu kuwaletea wakazi kipato zaidi. Picha/ Richard Maosi

Alisema kuwa atatumia hela hizo kuchonga mizinga ya kisasa ili kuongeza idadi ya nyuki wanaozalisha asali, ikiaminika kuwa soko la bidhaa hii ni kubwa kuliko kiwango kinachozalishwa humu nchini.

Aliwashauri vijana kuna nafasi nyingi za ajira katika sekta ya kilimo,na ujasiria mali ndio njia ya kipekee kupambana na ukosefu wa ajira

Alisema hii ni njia moja ya kuwakwamua wakulima wadogo mashinani waliosahulika,nao waanze kujinufaisha na ukulima.

Alieleza kuwa mradi wenyewe utakuja na faida nyingi ikiwemo kuboreshewa barabara,kupata soko la haraka na ajira kwa wakulima wanaotegemea mikopo kabla ya kujianzishia miradi.

Kampeni yenyewe ni katika hatua ya serikali kutimiza ajenda zake kuu,ifikapo 2022,mojawapo ikiwa ni taifa kuzalisha chakula cha kutosha kulisha raia wake.

You can share this post!

Polisi anayechunguza kesi ya Alai aitwa kortini

SADFA: Ezekiel Mutua asimulia kuugua kwa babake huku naye...

adminleo