Habari

Kura ya Olunga yapaisha Vinicius Junior kutawazwa Mwanasoka Bora Duniani wa FIFA

Na GEOFFREY ANENE December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

VINICIUS Junior hatimaye amepata kuwa namba wani duniani baada ya kutawazwa Mwanasoka Bora Duniani wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwenye hafla iliyofanywa jijini Doha, Qatar, Jumanne usiku.

Mbrazil huyo, ambaye alimaliza wa pili nyuma ya Mhispania Rodri katika tuzo ya Mwanasoka Bora Duniani ya Ballon d’Or licha ya kupigiwa upatu mwezi Novemba, alizoa pointi nyingi kuliko wapinzani wake wa karibu.

Vinicius asherehekea na kombe la UEFA baada ya timu yake ya Real Madrid kuibuka bingwa uwanjani Wembley jijini London, Uingereza, mnamo Juni 01, 2024. PICHA | REUTERS

Winga huyo wa Real Madrid alipata pointi 48 akifuatiwa na mshindi wa Ballon d’Or, Rodri, anayechezea Manchester City (43).

Kisha Muingereza Jude Bellingham wa Real Madrid (37), Dani Carvajal (31), Lamine Yamal (30), Lionel Messi (25), Toni Kroos (18), Erling Haaland (18), Kylian Mbappe (14), Florian Wirtz (nane) na Federico Valverde (nne) wakafuatana katika usanjari huo.

Manahodha wa timu za taifa akiwemo Mkenya Michael Olunga walipiga kura kuchagua mchezaji bora. Olunga pamoja na manahodha wa Burundi, Djibouti, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Uganda walimpigia kura Vinicius. Mbwana Samatta (Tanzania) na Bizimana Djihad (Rwanda) walianguka na Rodri.

Mbali na manahodha, makocha, wanahabari na mashabiki pia walipiga kura.

Nahodha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Micheal Olunga, mjini Nairobi awali Mei 2024. PICHA | CHRIS OMOLLO

Vinicius Junior ni Mbrazil wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu ianzishwe mwaka 2016 akifuatwa nyanyo za Cristiano Ronaldo (2016 na 2017), Luka Modric (2018), Lionel Messi (2019, 2022 na 2023) na Robert Lewandowski (2020 na 2021).

Mshindi mara mbili wa Ballon d’Or ya wanawake, Aitana Bonmati alihifadhi tuzo yake ya FIFA kwa pointi 52 dhidi ya Mzambia Barbra Banda (39) na Caroline Hansen kutoka Norway (37).

Carlo Ancelotti (Real Madrid) na Emma Hayes (Chelsea/Amerika) waliibuka makocha bora wa kiume na kike, mtawalia. Tuzo za kipa bora mwanamume na mwanamke ziliwaendea Emiliano Martinez (Argentina na Aston Villa) na Alyssa Naeher (Amerika na Chicago Red Stars), mtawalia.