Makala

Wafanyakazi 200,000 wa matatu wapinga hatua ya kutaka kuwafurusha CBD

Na RICHARD MUNGUTI October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI zaidi ya 200,000 walioajiriwa na Vyama 12 vya Matatu wameomba Mahakama Kuu ya Milimani itupilie mbali kesi itayoipa serikali ya Kaunti ya Nairobi uwezo wa kuwafurusha kutoka vituo wanakobebea abiria.

Mawakili wa vyama hivyo wameeleza magari hayo ya abiria yanahudumia wakazi wa kaunti zaidi ya 15 nchini na kufurushwa kwao katikati mwa jiji kutasababisha mtafaruku mkuu na mihemko katika lingo za kisiasa.

Na wakati huo huo makampuni matatu ya kuuza mafuta ya petroli pia yamepinga hatua ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuyaamuru yafunge biashara zao hadi pale yatakapofuata sheria za mamlaka ya mazingira –Nema na mamlaka ya huduma ya mafuta ya petroli-Epra.

Mahakama kuu imefafanuliwa kwamba kufurushwa kwa matatu kutapelekea wafanyakazi zaidi ya 200,000 kupoteza kazi.

Mbali na familia na jamii kuathiriwa na hatua hii inayotokana na ubinafsi wa baadhi ya madiwani wa bunge la kaunti ya Nairobi walioitishwa hongo ya Sh2milioni ili wasipeleke mswada wa kutimuliwa kwa matatu hizi na biashara za mafuta ya petroli kufungwa, serikali kuu itakosa ushuru wa Sh2bilioni.

Wenye magari haya walidokeza kwamba kila mwaka wanalipa kaunti ya Nairobi kodi ya Sh200milioni.

Kila mwezi vibao vinavyowekwa kwenye paa za magari ya matatu zikionyesha kule gari inaenda vinalipiwa Sh15,000 kila mwezi kwa kaunti.

“Ni unafiki na ulafi wa hali ya juu wa madiwani kutaka hongo wanaotaka magari haya yafurushwe,” mawakili wanaowakilisha wahudumu hawa wanadai katika stakabadhi zao mahakamani.

Wahudumu hawa wa vyama hivi wameeleza mahakama kuu kwamba magari yao huwahudumia wakazi wa maeneo ya kaunti za Murang’a, Embu, Kirinyaga,Machakos, Makueni, Kisii, Nyamira, Kitale, Kisumu, Mombasa na Kakamega

Makampuni ya mafuta yaliyoshtakiwa ni Total Energies (Rhino), Ola Energy (Afya Centre) na Ola Energy (Afya Centre).

Walalamishi waliowasilisha kesi wakiomba makampuni haya ya mafuta yafungwe ni Ezekiel Oyugi na Joshua Karuu.

Oyugi na Karuu wameshtaki pia Serikali ya Kaunti ya Nairobi (NCC).

Vyama vya matatu vilivyoshtakiwa (Sacco) ni: Ena Investiment Limited, Transline, Prestige, Kinatwa, Kam, Makos, Thika Road, Muna, Kamuna, Kangema Travellers, Libera Impex Empire, Inter-County Travelers, Muna Shuttle Limited, Kigumo T, Supreme T & T, GTS Supreme, Matco na Nnus Shuttle.

Mahakama imeelezwa na wenye matatu hawa kwamba maisha yao na yale ya watu wanaowategemea ikiwa ni pamoja na Mekanika, makampuni ya kuuza magurudumu ya magari yatapata hasara kuu isiyopungua Sh10bilioni.

Mawakili Danstan Omari na Stanley Kinyanyui wanaowakilisha wahudumu hawa wameomba mahakama kuu izingatie maslahi ya familia zinazotegemea matatu hizi.

Mahakama imeorodhesha kesi hii kusikizwa Januari 26,2026.

Magari ya Sacco hizi yalifikishwa kortini na wahudumu hawa wanaomba jaji anayesikiza kesi hii atembelee maeneo wanayohudumia ashuhudie kama kuna uchafu na ikiwa shughuli zao zinahatarisha maisha ya umma kama inavyodaiwa na Oyugi na Karuu.