Baada ya Nairobi, Ruto atarajiwa kuzuru Mlima Kenya
RAIS William Ruto anatarajiwa kuzuru eneo la Mlima Kenya katika wiki chache zijazo, huku maandalizi yakiendelea kwa kasi.
Ziara hii itakuwa ya kwanza ya maendeleo katika eneo hilo tangu kutimuliwa kwa Bw Rigathi Gachagua kama naibu rais mnamo Oktoba mwaka jana, hatua iliyogawanya eneo hilo lenye kura nyingi kati ya wafuasi wa washirika hao wawili waliogeuka kuwa mahasimu.
Rais Ruto alipata uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo kupitia chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kwenye uchaguzi wa Agosti 2022, huku wapiga kura wakimkataa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na chaguo lake la mrithi, Bw.Raila Odinga. Ruto alipata asilimia 47 ya kura zake milioni 7.2 kutoka eneo hilo.
Baada ya kufutwa kazi kwa Bw Gachagua na Prof Kithure Kindiki kuchukua nafasi yake, Gachagua alianzisha kampeni dhidi ya aliyekuwa bosi wake, akimshutumu kwa usaliti na kudai kuwa hakutetea maslahi ya jamii hiyo. Ameapa kuhakikisha kuwa Rais Ruto anakuwa kiongozi wa muhula mmoja huku akijiandaa kuzindua chama chake cha siasa mnamo Mei.
Hata hivyo, washirika wa Rais Ruto wakiongozwa na Prof Kindiki wamemtetea wakisema kuwa aliyekuwa Naibu Rais alishindwa kutimiza jukumu lake la kuimarisha umoja wa Wakenya.
Katika maandalizi ya ziara hiyo, Prof Kindiki Alhamisi alifanya mkutano wa mashauriano na wabunge 54 kutoka eneo hilo katika makazi yake ya Karen, ambapo aliwataka viongozi kuwa tayari kumpokea Rais.
Wabunge hao walitoka katika kaunti za Laikipia, Nyandarua, Nakuru, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Embu, Meru, na Tharaka Nithi. Ajenda ya mkutano ilikuwa kufuatilia maendeleo ya miradi ya serikali na utekelezaji wa mipango ya serikali ya kitaifa.
Mkutano huo pia ulikuwa kufuatilia ule uliofanyika Machi 6, ambapo Naibu Rais aliandaa kikao na wabunge kutoka maeneo yanayokuzwa kahawa ili kujadili mageuzi na mbinu za kuboresha mapato.
Mazungumzo yalihusu kuondoa vikwazo vinavyolemaza utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo.
Katika mkutano huo wa Karen, wabunge walifahamishwa kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Kitaifa kupata rasilimali za kukamilisha barabara ambazo ujenzi umekwama, zikiwemo barabara za Mau Mau, barabara kuu ya Kenol-Marwa, mabwawa makubwa ya kuongeza usambazaji wa maji na unyunyuzaji na ujenzi wa masoko.
“Tulielezwa pia kuhusu sera na hatua za kiutawala zilizochukuliwa na serikali kufufua mifumo ya thamani ya mazao kama chai, kahawa, maziwa, mpunga, viazi, macadamia, miraa, muguka, na kuku,” alisema mbunge mmoja aliyehudhuria mkutano huo.
Mbunge wa Imenti ya Kati, Bw Kirima Ngucine, aliyekuwa kwenye kikao hicho, alithibitisha kuwa Rais atazuru eneo hilo kuzindua miradi kadhaa.
“Ndiyo, tunajiandaa kwa ziara ya Rais, lakini bado hatujapewa tarehe kamili na ratiba ya ziara hiyo,” Bw Ngucine aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu, akiongeza kuwa Rais atazindua miradi iliyo na ufadhili tayari.
Katika hotuba yake ya awali, Prof Kindiki alisema hawataruhusu Rais kudhalilishwa kwa kuzindua miradi itakayokwama baadaye.
“Nitafanya kazi na mawaziri na maafisa wengine husika ili kuhakikisha kuwa kila mradi utakaozinduliwa na Rais una bajeti yake. Hatutaki aibu ambapo Rais anazindua mradi kisha unasimama katikati,” alisema naibu rais.
Mbunge mwingine kutoka Meru alisema kuwa Rais Ruto atazuru eneo hilo katika muda wa wiki tatu zijazo. “Miradi itakayozinduliwa bado haijakamilika kuchaguliwa, na hilo ndilo tunalofanyia kazi,” alisema mbunge huyo.