Mganga mashakani ndumba zake kushindwa kunasa vipusa
KORINDA, BUSIA
Na DENNIS SINYO
MGANGA mmoja mtaani hapa alitoroka sokoni baada ya wateja wake kumvamia kutaka kumchapa wakidai alikuwa akiwachezea shere.
Jamaa huyo alikuwa sokoni kwenye mishemishe za kutafutia familia posho wakati vijana wawili walipofika na kumfokea. Vijana hao walidai alikuwa amewatapeli Sh10,000 kwa kuwauzia hirizi bandia. Walidai jamaa huyo aliwashawishi kwamba alikuwa na dawa za kuwawezesha wajipatie vidosho bila kutoa jasho.
Vijana hao waliamua kumpa jamaa huyo hela zao na kisha akawapa hirizi kuvalia kila mara wanapowaona vidosho hao. Licha ya kuhakikishiwa matokeo mazuri, vijana hao walitamauka ndumba zilipokosa kufanya kazi.
Kijana wa kwanza alidai alifuata maagizo ya kalameni lakini nusura ajitie mashakani. Alidai kipusa aliyekuwa akimezea mate alimgeukia na kutaka kumchapa kofi mbele ya watu.
“Wewe ni mkora sana. Unakula pesa zetu eti unatupa dawa kumbe ni uongo,’’ alifoka kijana huyo. Kijana wa pili naye alichemka vikali pia akidai alichezwa shere.
Vijana hao walitaka kumpa jamaa kichapo wakitaka kurudishiwa pesa zao. Hata hivyo alifaulu kupenyeza kwenye umati na kuhepa ili kuepuka gadhabu za watu. Jamaa huyo alikuwa akitumia ujanja kuwatapeli wakazi.