Makala

Kaa chonjo, kuna mvua katika maeneo haya wikendi

Na BENSON MATHEKA February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUTAKUWA na mvua katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Nakuru, na Machakos wikendi, kulingana na utabiri wa hivi punde wa hali ya hewa.

Katika utabiri wa hali ya hewa wa siku tano zijazo, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa  Kenya ilitangaza uwezekano wa mvua kunyesha katika maeneo machache katika Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, Nyanda za Chini Kusini-Mashariki, na Bonde la Ziwa Victoria.

Kulingana na utabiri wa kipindi cha kuanzia Jumamosi, Februari 8, hadi Jumatano, Februari 12, 2025, Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, zikiwemo Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, na Tharaka, zilitarajia kupata mvua.

Utabiri huo unaeleza kwamba  kutakuwa na mvua Jumapili alasiri huku maeneo hayo yakitarajiwa kuwa na jua asubuhi na mawingu kiasi usiku. Wiki ijayo, Jumatatu hadi Jumatano,  kutakuwa na jua asubuhi na alasiri na mawingu kiasi usiku katika maeneo hayo.

Katika  Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, na eneo pana la Bonde la Ufa—ambalo linajumuisha kaunti kama Kisumu, Kisii, Uasin Gishu, Nakuru, Kakamega, na Busia, utabiri unaonyesha  kutakuwa na  mvua mchana na usiku mnamo Jumamosi na Jumapili.

Kulingana na utabiri huo, kutakuwa na mvua Jumatatu asubuhi katika maeneo machache na usiku pia. Jumanne asubuhi pia inatabiriwa kuwa na mvua, huku siku iliyosalia ikitarajiwa kuwa na jua na mawingu kiasi. Hakuna mvua iliyotabiriwa Jumatano katika maeneo hayo.

Kaunti za Pwani, ikiwa ni pamoja na Mombasa, Kilifi na Kwale, zinatarajiwa kusalia kavu wakati wa mchana, huku kukiwa na mawingu mara kwa mara nyakati za usiku. Hata hivyo, Kwale inatarajiwa kupokea mvua siku ya Jumapili mchana.

Katika nyanda za kusini-mashariki, ikijumuisha kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, na Taita Taveta, na pia sehemu za bara za Kaunti ya Tana River, utabiri unaonyesha hali ya mvua siku za Jumamosi na Jumapili.

Kulingana na utabiri huo, mvua inatabiriwa kunyesha mchana na usiku katika maeneo yanayozunguka Kilimanjaro katika mpaka wa Kenya na Tanzania.

Kaunti za kaskazini-mashariki mwa nchi—Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo—zinaweza kutarajia vipindi vya jua asubuhi na alasiri, huku usiku ukitarajiwa kuwa na mawingu kiasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utabiri  Hali ya Hewa y Kenya, Dkt David Gikungu, amewatahadharisha wakazi katika maeneo ya kaskazini-magharibi na kaskazini-mashariki mwa nchi kuwa waangalifu kutokana na upepo mkali unaotarajiwa kutoka kusini-mashariki.