Dimba

UEFA: Kitaeleweka Man City na Real Madrid zikikutanishwa mchujo wa kuingia 16-bora

Na GEOFFREY ANENE, MASHIRIKA February 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MANCHESTER City wana kibarua kigumu kupita raundi ya 32-bora kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kukutanishwa na mabingwa watetezi Real Madrid, katika droo iliyofanywa Ijumaa.

Ni mechi itakayokutanisha baadhi ya wafumaji matata katika soka, Kylian Mbappe (Real) na Erling Haaland (City).

Katika droo hiyo ya mechi za mchujo kwa timu zilizokamilisha mkondo wa ligi katika nafasi ya tisa hadi 24, iliyofanywa mjini Nyon nchini Uswisi, Club Brugge watavaana na Atalanta nao Sporting CP wakabane koo na Dortmund.

Kevin De Bruyne (kushoto) na Erling Haaland (kulia) wa Man City wapambana na Antonio Rudiger wa Real Madrid, mechi ya UEFA ugani Santiago Bernabeu mnamo 2023. PICHA | AFP

Celtic watakuwa kikaangoni mwa Bayern Munich, Juventus na PSV Eindhoven wataonana uso kwa macho, Feyenoord watapimwa vilivyo na AC Milan, Brest vs Paris Saint-Germain katika mpepetano wa timu zote za Ufaransa, nao Monaco watakabiliana na Benfica.

Washindi wa mechi hizo nane wataingia 16-bora ambapo wanasubiriwa Liverpool, Barcelona, Arsenal, Inter Milan, Atletico Madrid, Bayer Leverkusen, Lille na Aston Villa waliofuzu kwa kumaliza mkondo wa ligi ndani ya nane-bora.

Kocha Pep Guardiola na vijana wake wa City walimaliza mkondo wa ligi – ulioshirikisha jumla ya timu 36 – katika nafasi ya 22 kati ya washiriki 36 nayo Real ya Carlo Ancelotti ikawa nambari 11.

City, ambao wametapatapa msimu huu ikiwemo kwenye Ligi Kuu (EPL), wameshinda UEFA mara moja – mwaka 2023. Mabingwa watetezi Real wanashikilia rekodi ya mataji mengi zaidi (15).

Kocha wa Man City, Pep Guardiola (kulia), na mwenzake wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, wakati wa mechi ya UEFA ugani Etihad mnamo 2023. PICHA | AFP

City na Real wamekutana katika Klabu Bingwa Ulaya mara 12 tangu mwaka 2012. Takwimu zinaonyesha Real wamepiga City mara nne, wakapoteza mechi nne na kupiga sare nne.

City wataanzia shughuli nyumbani mnamo Februari 11 uwanjani Etihad kabla ya kuzuru ugani Santiago Bernabeu mnamo Februari 18. Mshindi kati ya City na Real ataingia michuano ya 16-bora itakayofanyika mwezi Machi.

Kufikia sasa ni washambulizi Serhou Guirassy (Dortmund) na Robert Lewandowski (Barcelona) wanaoongoza ufungaji wa mabao UEFA msimu huu wakiwa wametetemsha nyavu mara tisa kila mmoja.