• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
Mwanasiasa yeyote asijiapishe tena kama Raila, ni haramu – Mudavadi

Mwanasiasa yeyote asijiapishe tena kama Raila, ni haramu – Mudavadi

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi amebadilisha msimamo wake kuhusu hatua ya Bw Raila Odinga (ODM) kujiapisha kama ‘Rais wa Wananchi’.

Mnamo Januari 30, 2018 katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi, Bw Odinga alikula kiapo katika hafla iliyoendeshwa na mawakili Miguna Miguna ambaye alifurushwa nchini kwa kuzindua vuguvugu la NRM, lililotajwa kuwa haramu, na TJ Kajwang.

Kinara huyo wa Nasa alichukua hatua hiyo baada ya kubwagwa na Rais Uhuru Kenyatta (Jubilee) katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2017.

Mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka (Wiper) na vinara Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Isaac Rutto (Chama Cha Mashinani) hata hivyo hawakuhudhuria hafla hiyo iliyotajwa kuwa haramu na ya uhaini ambayo adhabu yake kisheria ni kunyongwa.

Vinara hao waliunga mkono Bw Odinga kujiapisha kama ‘Rais wa Wananchi’, licha ya kutohudhuria.

Bw Mudavadi amebadilisha msimamo wake na kutaja hafla hiyo kuwa haramu na isiyopaswa kurudiwa tena katika historia ya Kenya.

Alisema yeye na vinara wenza walifahamu bayana kuwa ni ukiukaji wa sheria na Katiba na ndio maana hawakuhudhuria.

“Ulikuwa uapisho wa dhihaka na uliokiuka sheria na Katiba, ndiyo sababu hatukuhudhuria,” Bw Mudavadi akasema majuzi kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga.

Kiongozi huyo wa ANC na ambaye ni mwasisi wa Nasa alisema amekuwa kwenye serikali kwa muda mrefu, na asingehudhuria hafla inayokiuka sheria za nchi.

“Hafla ya aina hiyo haitambuliwi hapa nchini na katika mataifa ya kigeni. Ilikiuka Katiba na haipaswi kurudiwa tena,” akasema.

Bw Mudavadi amekuwa akimhimiza Raila Odinga kuunga azma yake kuingia Ikulu 2022, ila Odinga amenukuliwa akiwasuta vinara wenza katika Nasa akiwataja kama wasaliti kwa kukosa kuhudhuria uapisho wake.

You can share this post!

Magavana wataka watengewe fedha za kufadhili afya, kilimo...

Poleni mashabiki, yalikuwa tu majaribu ya kimwili –...