• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
DINI: Usiogope kushindwa, hiyo ni kama giza kabla ya pambazuko

DINI: Usiogope kushindwa, hiyo ni kama giza kabla ya pambazuko

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Kinyume cha kushinda si kushindwa. Kushindwa ni sehemu ya mchakato wa kushinda. Kushindwa ni mafanikio safarini.

Albert Einstein katika mtazamo huu alisema, “Kushindwa ni mafanikio katika mwendo wa mbele.’ Kushindwa ni mafanikio katika hatua fulani. Kabla ya mapambazuko huwa kuna giza sana. Hapo unajua mapambazuko hayako mbali.

Tunasoma hivi katika Biblia, ‘Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; nikiwa gizani, Mwenyezi – Mungu ni mwanga wangu’ (Mika 8: 7).

Kuna ambao ukishindwa wanafurahia.Habari njema ni kuwa ushindi ni mbele kwa mbele. Ukishindwa unaweza kusema, ‘mtaijua jana yangu.’

Jana yako ilikuwa ni maandalizi ya ushindi. ‘Kushindwa ni kushinda kama tutajifunza kutokana na kushindwa,’ alisema Malcom Forbes. Kushindwa ni kuwa katika giza. Kushinda ni kuwa katika mwanga.?Usikate tamaa kushindwa ni giza linalotangulia mapambazuko.

Bashiri huyu ni nani? Alishindwa katika biashara mwaka 1831. Alishindwa kuwa mmojawapo wa watunga sheria mwaka 1832. Alishindwa katika biashara tena mwaka 1833.

Alichaguliwa kuwa mmojawapo wa watunga sheria mwaka 1834. Mpendwa wake wa moyo yaani mke wake aliaga dunia mwaka 1835. Alichanganyikiwa mwaka 1836. Alishindwa nafasi ya spika mwaka 1838. Alishindwa kuchaguliwa kuwa ‘Elector’ mwaka 1840.

Alishindwa kuingia kwenye Congress mwaka 1843, alishindwa tena kuingia kwenye Congress mwaka 1846. Alishindwa tena kuingia kwenye Congress mwaka 1848.

Alishindwa kuwa Seneta mwaka 1858. Alichaguliwa kuwa rais wa Marekani mwaka 1860. Jina chini ya rekodi hii ni Abraham Lincoln. Kushindwa kwake lilikuwa ni giza lililotangulia mwanga.Ijumaa kuu ni giza. Jumapili ya Pasaka ni mapumziko.

Siku ya Ijumaa Kuu, ‘….tangu saa sita palikuwa ni giza juu ya nchi yote hata saa tisa’ (Mathayo 27: 45). Ijumaa Kuu ni siku ya giza. Jumapili ya Pasaka ni siku ya mwanga. Ijumaa Kuu ni kushindwa. Jumapili ya Pasaka ni kushinda. Yesu alizishinda nguvu za giza.

Alisema, ‘Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu’ (Yohane 16: 33). Tumefanya urafiki na ushindi tumtazame yeye. Tambua nguvu ya maneno ya Yesu, ‘nimewaita rafiki.’ Neno ‘rafiki,’ linavunja vizuizi vingi.

Kuna hadithi juu ya mkulima ambaye alijaribu kumfundisha kijana wake kulima kwa Plau. Plau ni chombo Cha kulima kinachovutwa na trekta au mnyama.

Baada ya farasi kufungwa vizuri na kila kitu kilikuwa tayari, alimwambia kijana wake kumtazama ng’ombe huyo. Kijana alianza kulima kwa plau.

Aliporudi alishangaa. Mstari ulikuwa unafanana alama ya kuuliza. Kijana alifuata maelekezo. Shida ng’ombe alitoka alipokuwa amelala.

Yesu ni mwamba habadiliki. Mtazame yeye.Kushindwa ni giza linalotangulia mapambazuko. Ukipanda maarage kwenye udongo wenye mbolea yanakuwa gizani. Baadaye yanaota.

Giza linatangulia mapambazuko. Mungu Baba aliwapa Yesu na Lucifer mtihani wa kutumia kompyuta. Shetani ‘alitaipu’ kwa spidi kubwa lakini bila ‘kusevu’ bila kudunduliza maneno anayoyataipu.

Yesu alifungua faili na kulipa jina. Alipiga taipu na kusevu. Umeme ulikatika dakika mbili. Baada ya umeme kurudi waliambiwa kuchapa.

Kwa Yesu ilikuwa rahisi. Shetani alishindwa na kulalamika, andiko lilipotea. Mungu Baba alimwambia Shetani, ‘Yesu anaokoa'(Jesus saves).Kuna aliyesema, ‘Kama hitaji letu kubwa sana lingekuwa habari, Mungu angetutumia mwanahabari. Kama hitaji letu kubwa sana lingekuwa teknolojia Mungu angetumia mwanasayansi.

Kama hitaji letu kubwa sana lingekuwa pesa Mungu angetutumia mchumi. Kama hitaji letu kubwa sana lingekuwa raha Mungu angetutumia Mwokozi.

You can share this post!

Magavana waunda vyama vipya kuepuka baridi 2022

Koome aagiza kesi za miaka minne zimalizwe