• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
OMAUYA: Kauli ya Ruto: ‘nichukie ila swara tutamla hadi tamati’

OMAUYA: Kauli ya Ruto: ‘nichukie ila swara tutamla hadi tamati’

Na MAUYA OMAUYA

JE, ni lipi afadhali kati ya ndoa mbaya na ukapera mwema?

Huo ndio uamuzi wa kisiasa unaomkabili Naibu wa Rais William Ruto huku uhusiano wake na bosi wake ukizidi kuzorota na tofauti zao kudhihirika kwa maneno na vitendo. Kufaulu kwa BBI kwenye mabunge ya kaunti kumevuruga zaidi anga ya Dkt Ruto kwenye chama tawala cha Jubilee.

Mahasidi watatumia kila fursa kumdhihaki Ruto na iwapo kura ya maoni kuhusu BBI itatumiwa kama kigezo cha umaarufu wa sera, basi wataitumia kuzima na kuchakiza azma yake ya kutwaa ikulu ifikapo uchaguzi wa mwaka 2022.

Talaka rasmi kati ya Uhuru na Ruto sio jambo rahisi. Ilivyo kikatiba kwa sasa, Uhuru hawezi kumtimua kwa kumfuta kazi. Mbinu ya kwanza ni kumng’oa afisini kupitia mswada bungeni lakini hatua hii itaibua uhasama na joto kali la kisiasa ambalo litaathiri mno shughuli na utendakazi wa serikali na utulivu wa taifa. Inawezekana pia hatua hii isipate uungwaji mkono na idadi inayotakikana ya wabunge.

Pili, Dkt Ruto anaweza kujiondoa mwenyewe kwa kujiuzulu. Akufukuzaye hakwambii toka. Hata hivyo, Uhuru ameonyesha ishara dhahiri kwa kumtenga, kumnyima majukumu na zaidi ya yote amenena kwa kinywa chake. Ruto naye bila kusema waziwazi hadharani, anaendesha shughuli mbadala kwa kujipigia debe, kupinga BBI, kushtumu baadhi ya sera za serikali na kuzindua chama cha UDA kama chombo kipya cha kisiasa.

Mienendo na azma zake zinakinzana na za Rais, gundi iliyowaweka pamoja imeyeyuka. Hakuna urafiki, matamshi yao kwa umma ni diplomasia ya unafiki tu, kuendelea kufumba raia macho. Uhuru ameshindwa kumtimua, naye Ruto amenata, hatoki kwa hiari yake.

Yaelekea msimamo wa Ruto ni: Tuliwinda huyu swara sote, tukapika sote na mnofu na kitoweo tutakula sote hadi tamati. Tutabanana hapa hapa, utakula kulia nami nile kushoto, yetu mamoja. Aliyekupa urais, alinifanya pia naibu wa rais. Sote tuna haki sawa. Kama uko ndani, nami niko ndani. Sitoki kwa vitisho, nitatoka nikitaka! mkivileta vya kuleta, mimi niko tayari, niko fiti kishenzi!”

Makamu wa rais wa kwanza, Jaramogi Oginga Oginga alipotofautiana na Mzee Jomo Kenyatta, alijiuzulu na kuondoka serikalini kisha akaunda chama cha KPU mwaka was 1966. Raila Odinga naye aliwahi kujiuzulu kutoka bungeni alipozozana na uongozi was chama cha Ford Kenya. Falsafa ya Ruto ni tofauti, moyo na imani yake iko kwenye chama cha UDA lakini anabaki naibu rais chini ya serikali ya Jubilee. Huu ni mchezo wa kaka mbweha na fisi porini na hakuna mwongozo wa demokrasia hata kidogo. Hana ujasiri

Ikiwa naibu wa rais anaamini ana wabunge wa kutosha, ingefaa ajiondoe pamoja na wabunge hao ili kulazimisha uchaguzi mpya. Hawezi kwa sababu siasa za wabunge hawa haziongozwi na misimamo thabiti. Woga wa kumwaga unga unazidi mapenzi yao kwa UDA na Ruto. Isitoshe, Ruto mwenyewe hana hakika maisha yatakuwa vipi nje ya kasri lake na ofisi yake rasmi. Wakitazama yanayompata Sonko baada ya kupoteza kiti, wengi wa viongozi hawa wanasalia kuduwaa.

Kwa kupinga BBI na kuzindua UDA, Ruto alitaraji kupima kina cha mto kwa mguu wake mmoja, gota gongo usikie mlio wake. Amegundua hatavuka mto huu kwa usalama, hali si shwari, atazama. Yaelekea, pindi tu William Ruto atakapojiondoa serikalini, ushawishi wake utayeyuka. Hangependa hilo hasa kabla ya 2022. Sasa yuko kwenye njia panda. Atazidi kuimba wimbo wa “..mimi kama naibu wa rais” hadi siku ile hali itamfaa.

Hali ndio hii kwenye ndoa ya machozi; Uhuru amemkazia boriti Ruto “utaishia kunawa bibi, hatuli sahani moja.” Naye Ruto anajipa moyo, “tutabanana hapa hapa ……ndoa mbaya ni afadhali kuliko ukapera mwema”.

[email protected]

You can share this post!

MATHEKA: BBI inafaidi wanasiasa pekee mzigo ukiwa kwa raia

TAHARIRI: Serikali isambaze nakala za Kiswahili