• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
VITUKO: ‘Marafiki pesa’ wamwandama Pengo baada ya kushinda malaki ya kamari

VITUKO: ‘Marafiki pesa’ wamwandama Pengo baada ya kushinda malaki ya kamari

Na SAMUEL SHIUNDU

TANGU apoteze pesa katika mchezo wa kamari miaka kadhaa iliyopita, hakuna yeyote kati ya jamaa na rafiki zake aliyesikia habari zake na kamari tena.

Alifananishwa na mtu aogopaye ung’ong’o baada ya kuumwa na nyoka. Ungemuuliza yeyote kama Pengo alishiriki kamari, ungejuzwa kuwa mwalimu kalitupa jongoo pamoja na jiti la kumkokotea. ‘Mwalimu huyo na kamari ni kama mafuta na maji.’ Wengine waliamini

Hawakujua kuwa Pengo aliendeleza kamari japo kisirisiri. Hakuna aliyeweza kumtuhumu kama mshiriki wa mchezo huo kwa sababu muda wote huo alikuwa akilaghaiwa na makampuni ya kamari. Pamoja na tabia za makampuni haya ya kamari za kuyabana majina ya wale wanaopoteza hela zao michezoni, ilikuwa vigumu kwa Pengo kugundulika kama mshiriki.

Pengo mwenyewe alifurahia usiri huo kwani hakutaka watu wajue kuwa mhubiri wa kiwango chake aliishiriki michezo ya aina hiyo hasa baada ya kupoteza maelfu awali.

Kwa hivyo mwalimu wa watu aliendelea kuhesabu hasara na kuyalaani makampuni hayo kimya kimya. Kila siku alijiahidi kuachana na kamari lakini alijipata akicheza siku baada ya siku.’Mazoea yana taabu aisee!’ alijiambia kila baada ya kupoteza.

Kwa hivyo basi Iliwashangaza wengi ilipotangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa Pengo wa Nzeki alikuwa kashinda laki kadhaa kwenye mchezo wa kamari wa kutabiri matokeo ya mechi. Simu na jumbe za pongezi kutoka kwa jamaa na marafiki zikaanza kumiminika simuni mwake. Baadhi ya watu ambao kabla ya hapo, hakujua uwepo wao walianza kujitokeza na kumshukuru. Wapo waliomkumbusha udugu wao, wengine wakaufufua urafiki uliokuwa umetupwa katika kaburi la sahau, almuradi Pengo aligeuka ghafla na kuwa mtu muhimu katika maisha ya wengi. Vikasha vya jumbe katika mitandao yake ya kijamii navyo vikajaa jumbe za kila aina kutoka kwa wanaume na wanawake. Nyingi lakini zilitoka kwa wanawake.

Ilimuwia vigumu kujibu jumbe hizi zote. Akateua chache tu za kujibu. Mmoja wa wale waliobahatika kujibiwa alikuwa mwanadada aliyejiita Lazizi Penzi. Pengo hakumjua lakini uso wake na jina lake vilimvutia. Laiti angalijua kuwa huko kumjibu huyo Penzi kulikuwa sawa na kujipalia makaa!

“Nirushie kitu kidogo. Niko kazini usiku wa leo na sina chajio” Lilikuja ombi ambalo Pengo hakutarajia.

“Wewe hufanya kazi gani?”Pengo aliuliza. “Mimi ni nesi,” Penzi akamjibu. Pengo alitamani kumwambia ale chajio cha wagonjwa. Lakini badala yake akamwambia kuwa nesi walipokea mishahara mikubwa kuliko walimu. Mawasiliano yakakatika.

You can share this post!

Bruno Fernandes atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa...

TAHARIRI: Sasa serikali ifufue ajenda ya chakula