• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Barcelona kusajili wanasoka saba wapya baada ya kocha Koeman kupata kibali cha rais mpya Joan Laporta

Barcelona kusajili wanasoka saba wapya baada ya kocha Koeman kupata kibali cha rais mpya Joan Laporta

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman amefichua mipango ya kusajili wanasoka saba wakiwemo Memphis Depay, Erling Haaland, Romelu Lukaku, Georginio Wijnaldum na Eric Garcia mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Hii ni baada ya mkufunzi huyo raia wa Uholanzi kuhakikishiwa na rais mpya wa Barcelona, Joan Laporta, kwamba mkataba wake wa kuhudumu uwanjani Camp Nou utarefushwa.

Koeman ambaye kwa sasa angali na mwaka mmoja pekee kwenye kandarasi yake na Barcelona, amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuondoka na mahali pake kutwaliwa ama na Mikel Arteta wa Arsenal au Xavier Hernandez ambaye kwa sasa anawatia makali wanasoka wa Al-Sadd nchini Qatar.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Koeman amesema kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kumdumisha Lionel Messi uwanjani Camp Nou, kuhakikisha kwamba fowadi Ousmane Dembele anatia saini mkataba mpya na kushawishi Barcelona kujitwalia huduma za wanasoka saba wapya kwa ajili ya muhula ujao wa 2021-22.

Wijanldum anayetarajiwa kuondoka Liverpool anamezewa mate na Koeman kwa matumaini kwamba atafufua makali ya safu ya kati na kuendeleza ushirikiano mkubwa ambao umekuwapo kati yake na Depay katika timu ya taifa ya Uholanzi. Depay kwa sasa anachezea Olympique Lyon ya Ufaransa.

Garcia ni beki wa Manchester City nao Haaland na Lukaku wanasakatia Borussia Dortmund (Ujerumani) na Inter Milan (Italia) mtawalia.

Mkataba kati ya Barcelona na Messi unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na fowadi huyo raia wa Argentina anahusishwa na uwezekano wa kutua Man-City au Paris Saint-Germain (PSG). Kandarasi ya Dembele ugani Camp Nou inakatika mnamo Juni 2022.

Kusajiliwa kwa Garcia kunachochewa na haja ya Koeman kujaza pengo litakaloachwa na Junior Firpo ambaye amethibitisha kuondoka kwake kambini mwa Barcelona mwishoni mwa msimu huu.

Barcelona wamefichua mpango wa kumkweza ngazi chipukizi Alejandro Balde, 17, hadi kikosi cha kwanza baada ya kuridhisha zaidi katika akademia. Hatua hiyo itamwezesha kushirikiana vilivyo na Garcia iwapo juhudi za Barcelona kumsajili David Alaba kutoka Bayern Munich zitaambulia pakavu.

Baada ya kuaga mapema kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, Barcelona wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Kombe la Copa del Rey chini ya Koeman muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AC Milan wavunja benki ili kumsajili beki Fikayo Tomori...

KCSE: Waziri aonya wanafunzi wa vyuo