• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
Kocha Pioli imani tele kwamba Zlatan Ibrahimovic atarefusha mkataba wake AC Milan

Kocha Pioli imani tele kwamba Zlatan Ibrahimovic atarefusha mkataba wake AC Milan

Na MASHIRIKA

KOCHA Stefano Pioli wa AC Milan sasa amemtaka mshambuliaji mkongwe raia wa Uswidi, Zlatan Ibrahimovic kurefusha mkataba wake na kikosi hicho.

Ibrahimovic alifikisha jumla ya mabao 501 kapuni mwake mnamo Februari 7, 2021 kutokana na soka ya kitaaluma ambayo amekuwa akipigia klabu mbalimbali. Hii ni baada ya kupachika wavuni mabao mawili na kusaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 4-0 dhidi ya Crotone.

Kufikia sasa, Ibrahimovic anajivunia mabao 16 kutokana na michuano 17 ambayo amechezea AC Milan katika mashindano yote ya msimu huu.

Mkataba wa sasa kati ya Ibrahimovic na AC Milan unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na kocha Pioli ana wingi wa matumaini kwamba sogora huyo atarefusha muda wa kuhudumu kwake ugani San Siro.

“Sijui mipango yake lakini nina imani atasalia kuwa nasi. Ibrahimovic angali anatamba na amekuwa kiini cha ushindani mkali ambao kwa sasa tunashuhudia kikosini,” akasema Pioli.

“AC Milan ni timu kubwa ambayo ina kiu ya kufanya vyema katika soka ya Italia na bara Ulaya kama ilivyokuwa zamani. Ibrahimovic ana uwezo mkubwa wa kutuongoza kuyafikia malengo hayo,” akaongeza kocha huyo raia wa Italia.

Ibrahimovic kwa sasa anajivunia mabao 14 ligini na ndiye wa pili katika orodha ya wafungaji bora wa Serie A inayoongozwa na Cristiano Ronaldo ambaye ametikisa nyavu za wapinzani mara 16 kutokana na mechi 22 zilizopita.

Ibrahimovic aliyerejea AC Milan mnamo Janauri 2020, sasa amefunga magoli 27 kutokana na mechi 37 zilizopita akivalia jezi za waajiri wake na maazimio yake ni kushindia kikosi hicho ubingwa wa taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 msimu huu.

Mengi ya mabao 501 ambayo sasa yamefungwa na Ibrahimovic yalipatikana wakati akivalia jezi za kikosi cha Malmo FC kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uswidi. Nyota huyo alichezea Malmo yapata miaka 21 iliyopita kati ya Oktoba 1999 na 2001.

Ibrahimovic amewahi pia kuchezea klabu za Juventus, Ajax, Inter Milan, Barcelona, Paris Saint-Germain (PSG), Manchester United na LA Galaxy.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kang’ata avuliwa madaraka kwa kuanika barua...

BI TAIFA FEBRUARI 9, 2021