• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Lewandowski avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye Bundesliga katika mechi ya mwisho ya msimu huu

Lewandowski avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye Bundesliga katika mechi ya mwisho ya msimu huu

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Robert Lewandowski alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili katika mchuano wa mwisho wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu na kuvunja rekodi ya ufungaji wa magoli iliyokuwa ikishikiliwa na Gerd Muller kwa miaka 49.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland alitikisa nyavu za FC Augsburg katika dakika ya 90 na kusaidia waajiri wake Bayern Munich kusajili ushindi wa 5-2 katika mchuano huo.

Goli hilo la Lewandowski lilikuwa lake la 41 katika Bundesliga msimu huu. Ndiye kwa sasa anashikilia rekodi ya kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika msimu mmoja wa Bundesliga.

Lewandowski kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 53 kutokana na mechi 46 zilizopita katika ngazi ya klabu na timu ya taifa. Ni ufanisi unaotarajiwa kumpa motisha zaidi ya kutambisha Poland kwenye kampeni zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena, Bayern waliwafunga Augsburg jumla ya mabao manne katika kipindi cha kwanza huku kipa na nahodha wao Manuel Neuer akipangua mkwaju wa penalti.

Bayern ambao walijizolea taji la Bundesliga kwa mara ya tisa mfululizo msimu huu, walitumia mchuano huo kuaga kocha Hansi Flick pamoja na baadhi ya wanasoka watakaoagana nao muhula huu.

Flick aliyeajiriwa mnamo Novemba 2019, atabanduka kambini mwa Bayern baada ya kushindia kikosi hicho mataji mawili ya Bundesliga, ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), German Cup, Uefa Super Cup na Kombe la Dunia.

Mikataba kati ya Bayern na David Alaba pamoja na Javi Martinez inatamatika rasmi mnamo Juni 2021, sawa na beki Jerome Boateng aliyeondoka uwanjani akitiririkwa na machozi.

Hata hivyo, Lewandowski ndiye aliyeelekezewa macho zaidi huku juhudi zake za kuvunja rekodi ya ufungaji wa mabao zikizimwa mara kwa mara na kipa Rafal Gikiewicz wa Augsburg.

Baada ya kufunga bao, Lewandowski alivua jezi yake na kutoka nje ya uwanja kumkumbatia kocha Flick anayeondoka.

Mabao mengine ya Bayern yalifumwa wavuni na Serge Gnabry, Joshua Kimmich, Kingsley Coman na Jeffrey Gouweleeuw aliyejifunga.

Augsburg walifungiwa mabao yao na Andre Hahn na Florian Niederlechner baada ya Daniel Caligiuri kupoteza mkwaju wa penalti.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

JAMVI: Viatu vya urithi wa Uhuru vitatosha Muturi Mlimani?

Haaland abadilishana jezi na refa anayestaafu baada ya...