• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Uingereza na Scotland nguvu sawa kwenye pambano la Euro

Uingereza na Scotland nguvu sawa kwenye pambano la Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA na Scotland waliambulia sare tasa kwenye mchuano wa Euro wa Kundi D uliowakutanisha uwanjani Wembley mnamo Ijumaa usiku mbele ya mashabiki 22,500.

Licha ya kila mmoja kupoteza alama mbili muhimu, matokeo hayo yaliweka hai matumaini ya Uingereza na Scotland kusonga mbele na kutinga hatua ya 16-bora.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza tangu fainali za Euro 1996 kuwahi kukutanisha wanasoka wa kiume wa Uingereza na wa Scotland kwenye kivumbi cha haiba kubwa barani Ulaya.

Scotland walijibwaga ugani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupigwa 2-0 na Jamhuri ya Czech kwenye mchuano wa ufunguzi wa kampeni za makundi mnamo Juni 14, 2021 uwanjani Hampden Park.

Japo Uingereza walipigiwa upatu wa kutamba na kuwacharaza Scotland kirahisi, ubabe wao ulizimwa na nusura Scotland wakizamishe chombo chao katika kipindi cha pili.

Chini ya kocha Gareth Southgate, Uingereza walimtegemea sana kipa Jordan Pickford kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Stephen O’Donnell na Lyndon Dykes.

Presha hiyo ya Scotland iliwataabisha sana masogora wa Uingereza ambao licha ya utepetevu, walishuhudia fataki mbili kutoka kwa John Stones na Mason Mount zikigonga mwamba wa lango la Scotland.

Baada ya kushinda Croatia katika mchuano wao wa kwanza kwenye Kundi D, Uingereza kwa sasa wana fursa ya kuwaruka Jamhuri ya Czech iwapo watasajili ushindi katika mchuano wa mwisho wa makundi ugani Wembley. Scotland nao watakuwa wakiwinda alama tatu muhimu dhidi ya Croatia ugani Hampden Park mnamo Juni 22, 2021.

Ilikuwa mara ya nne kwa mechi kati ya Uingereza na Scotland ambao ni watani wao wakuu kukamilika kwa sare ya kutofungana tangu 1872, 1970 na 1987.

Sare tasa iliyosajiliwa na Uingereza ilikuwa yao ya kwanza kutokana na mechi 17 zilizopita kwenye kampeni za soka ya haiba kubwa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NMG yashirikiana na serikali ya Machakos kupanda miche...

Uswidi wapepeta Slovakia na kujiweka pazuri kuingia hatua...