• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Wakili Murgor akana vikali kuwa mkorofi

Wakili Murgor akana vikali kuwa mkorofi

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI Philip Murgor jana alijitetea vikali dhidi ya madai kwamba ni mkorofi na mkandamizaji haki, alipohojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu.

Alikana madai yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC) na walalamishi mbalimbali, akiwemo Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Nelson Havi.

Badala yake, Bw Murgor alisema yeye ni “mtetezi wa haki na kwamba Idara ya Mahakama inahitaji kuongozwa na mtu mkakamavu, shupavu, mjasiri na mchapa kazi kama yeye asiyeegemea upande wowote.”

Alihojiwa kwa undani jinsi alivyoshiriki katika kesi za mauaji ya mlowezi Tom Cholmondley; aliyekuwa Mbunge wa Kitutu Masaba marehemu George Moseti Anyona ambaye alishtakiwa mwaka 1991 pamoja na Prof Edward Akong’o Oyugi, aliyekuwa mhadhiri wa chuo kikuu Isaiah Ngotho Kariuki na Augustine Njeru Kathangu kwa uchochezi dhidi ya Serikali ya hayati Daniel arap Moi.

Kesi hizo na nyinginezo ziliwasilishwa mbele ya JSC na zinaonekana kutia ndoa fursa yake ya kuwa Jaji Mkuu.Pia alihojiwa kushiriki kwake katika maandamano ya mapinduzi ya Bw Moi mnamo 1982.

Bw Murgor alitiwa nguvuni pamoja na waandamanaji 60 na pia mwanajeshi marehemu Hezekiah Ochuka kufuatia jaribio la kumtimua mamlakani Bw Moi.

“Nilikamatwa na kufikishwa kortini kwa kushiriki katika maandamano ya mapinduzi ya serikali ya Bw Moi lakini nikaachiliwa kwa kukosekana ushahidi wa kuthibitisha nilikuwa mhalifu,” Bw Murgor aliungama.

Bw Murgor alisema licha ya kuwa alidhulumiwa na serikali ya Bw Moi aliifanyia kazi kwa moyo wa kujitolea.Bw Murgor alikuwa mwaniaji watano kuhojiwa na JSC.Alisema hatimaye serikali ya rais mstaafu Mwai Kibaki ilimwajiri kazi ya kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na hatimaye akajiuzulu alipotofautiana na maafisa wakuu serikalini.

Bw Murgor alisailiwa kuhusu kesi ya mauaji dhidi ya bwanyenye Kamlesh Pattni na kashfa ya kuwatimua kazini majaji na mahakimu wakati wa enzi ya marehemu Jaji Mkuu Evans Gicheru.

Bw Pattni, aliyewakilishwa na mwaniaji mwingine wa kiti hicho cha Jaji Mkuu Bw Fred Ngatia, aliachiliwa huru na Jaji Jessie Lesiit katika uamuzi uliozua utata.Bw Murgor aliomba JSC imteue kumridhi Jaji David Maraga aliyestaafu mwezi Januari.

Alisema akiteuliwa atahakikisha kwamba, “mahakama imepata ufanisi na kushauriana na Rais kuhusu kuapishwa kwa majaji 41 aliokataa kuwateua.”

Wakili huyo aliilaumu JSC kwa kutomuunga mkono aliyekuwa Jaji Mkuu Bw Maraga kuhusu suala la kuapishwa kwa majaji hao 41 na kupunguzwa kwa bajeti ya idara ya mahakama.Mahojiano ya Bw Murgor yalikumbwa na masuala chungu nzima huku akidai rais wa chama cha wanasheria nchini Nelson Havi amewasilisha madai ya uwongo na yasiyo na msingi.Bw Murgor alisema magenge ya wahalifu wanaohujumu idara ya mahakama yanapas kuangamizwa kabisa.

You can share this post!

Hatimaye Uhuru atangaza nafasi za makamishna IEBC

Afisa adai aliadhibiwa kwa kutopelekea Ruto umati