• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Inter Milan wapiga AC Milan na kufungua mwanya wa pointi nne kileleni mwa jedwali la Serie A

Inter Milan wapiga AC Milan na kufungua mwanya wa pointi nne kileleni mwa jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

MABAO mawili kutoka kwa fowadi Lautaro Martinez yalisaidia Inter Milan kupepeta watani wao AC Milan 3-0 kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) uwanjani San Siro, Jumapili.

Ushindi huo uliovunwa na masogora wa kocha Antonio Conte uliwawezesha Inter kufungua pengo la alama nne kati yao na nambari mbili AC Milan kileleni mwa jedwali. Kwa sasa wamejizolea jumla ya pointi 53 huku mwanya wa alama 10 ukitamalaki kati yao na Atalanta wanaofunga orodha ya nne-bora.

Martinez anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Barcelona mwishoni mwa msimu huu, aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao katika dakika ya tano kabla ya kufunga la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Fowadi wa Inter Milan raia wa Argentina Lautaro Martinez (kati-kushoto) asherehekea baada ya kumfunga bao kipa wa AC Milan Gianluigi Donnarumma wakati wa mechi ya Serie A katika uwanja wa San Siro mjini Milan, Februari 21, 2021. Picha/ AFP

Ingawa Zlatan Ibrahimovic alijitahidi kurejesha waajiri wake AC Milan mchezoni, juhudi zake ziliambulia pakavu baada ya makombora yake kudhibitiwa vilivyo na kipa Samir Handanovic aliyemnyima pia mfumaji Sandro Tonali nafasi kadhaa za wazi. Inter walifungiwa bao la tatu na fowadi wa zamani wa Everton na Manchester United, Romelu Lukaku katika dakika ya 66.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Aprili 2011 kwa Inter na AC Milan kukutana wakishikilia nafasi mbili za kwanza ligini.

Msimu huo, AC Milan waliwakung’uta Inter 3-0. Ushindi wa Februari 21 uliosajiliwa na Inter unawaweka pazuri zaidi kutawazwa mabingwa wa Serie A msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 2009-10.

Yalikuwa masikitiko makubwa kwa kipa Gianluigi Donnarumma wa AC Milan aliyekuwa akisakata mchuano wake wa 200 kwenye soka ya Serie A.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 21 ndiye mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kufikia rekodi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na kipa mkongwe wa Juventus, Gianluigi Buffon kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A sasa wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 42 japo wana michuano miwili zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimesakatwa na washindani wao wakuu wakiwemo Inter, AC Milan, AS Roma, Atalanta na Lazio.

MATOKEO YA SERIE A (Februari 21):

AC Milan 0-3 Inter Milan

Parma 2-2 Udinese

Atalanta 4-2 Napoli

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Messi aweka rekodi katika sare ya 1-1 kati ya Barcelona na...

Barabara ya Thika-Gatuanyaga kukamilika katika kipindi cha...