WARUI: Kazi kwenu sasa Jwan, Ruto kufanikisha mfumo wa CBC

Na WANTO WARUI

MABADILIKO yaliyofanywa juma lililopita na rais Uhuru Kenyatta katika wizara mbalimbali, yalinuiwa kuboresha utekelezaji wa majukumu na utendakazi katika serikali.

Mojawapo ya wizara ambazo zilipata mabadiliko makubwa ni ile ya Elimu ambapo Katibu Mkuu katika wizara hiyo Dkt Belio Kipsang na mwenzake naibu wa waziri Zack Kinuthia walihamishiwa kwingine. Dkt Kipsang alikuwa amehudumu katika wizara hii kwa muda mrefu wa miaka minane huku mwenzake Zack akiwa mbichi sana katika kuvitambua vyumba vya ndani vya Wizara ya Elimu.

Nafasi ya Dkt Kipsang imechukuliwa na Dkt Julius Jwan ambaye kabla ya kuhudumu katika TVET alikotolewa, alikuwa Mkurugenzi na afisa mkuu wa Taasisi ya Kuunda Mitaala Nchini (KICD). Nayo nafasi ya Bwana Zack ikachukuliwa na Dkt Sara Ruto ambaye alikuwa mwenyekiti wa baraza la KICD.

Mabadiliko haya yamekuja wakati ambapo Wizara ya Elimu inakumbwa na misukosuko kadhaa ikiwemo sintofahamu ya kuuendeleza mtaala mpya wa elimu, CBC. Ingawa Dkt Kipsang alikuwa amefanya mabadiliko katika sekta ya elimu kama vile kuanzisha NEMIS, suala la kupeana kompyuta katika shule za msingi lilimshinda na akafeli kabisa.

Kufikia sasa miaka miwili tu kabla Gredi ya nne haijatamatisha masomo yake ya shule ya msingi, serikali haijaunda sera mwafaka ya kuhakikisha mfumo huu wa CBC unafaulu. Bado walimu na wazazi wamo gizani wakisubiri kujionea ‘mpira utachezwa vipi’.

Huenda hofu hii pia ndiyo iliyomlazimisha rais kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu na kuleta watu ambao wanauelewa zaidi mtaala huu na ambao wamekuwa ndani yake tangu ulipoanzishwa.

Dkt Jwan amekumbatia sana mfumo wa CBC na amesikika mara kwa mara akiwashawishi walimu na wazazi wauunge mkono. Sasa amepata nafasi bora ya kuweza kutekeleza mabadiliko yafaayo katika sekta hii ya elimu. Bila shaka yeye pamoja na mwenzake, Dkt Sara Ruto, wataweza kumshauri Waziri wa Elimu kuhusu masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiathiri utekelezaji wa mfumo wenyewe na maendeleo ya elimu kwa ujumla.

Hata hivyo, hawa wawili wasitarajie kutembelea barabara isiyo na miba. Wizara hii ina changamoto tele ambazo zinaikumba kuanzia utovu wa nidhamu shuleni hadi ujenzi wa madarasa na ukosefu wa walimu wa kutosha shuleni.

Pamoja na kutekeleza mfumo huu mpya, Jwan na Ruto wanatarajiwa kusimamia utendakazi bora katika wizara, kuupisha mfumo wa 8-4-4 ipasavyo bila matatizo na kuukaribisha mfumo wa CBC vyema katika shule za sekondari.

Kufaulu kwa CBC bila shaka kutampa rais furaha akistaafu kwani itakuwa mojawapo ya sera ambazo zitapima kufaulu kwake katika utawala. Macho yote sasa yako kwa madaktari Jwan na Ruto.

Habari zinazohusiana na hii