Mechi za Kundi B NWRL zawaka moto

Na JOHN KIMWERE

MECHI za Kundi B kuwania Nairobi West Regional League (NWRL) ni miongoni mwa kampeni zinazoshuhudia ushindani wa kufa mtu msimu huu.

Kipute hicho kinajumuisha takribani timu 28 zinazopigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao. Red Carpet FC ni kati ya vikosi vinavyofukuzia tiketi za kupandishwa ngazi. Kocha wake, Meshack Osero Onchonga anasema ”Licha ya kuwa tunapitia changamoto za ukosefu wa fedha kugharamia shughuli zetu michezoni tunapania kujituma kiume kuwinda tiketi ya kuwa miongoni mwa vikosi vitakavyofuzu kusonga mbele.”

Hata hivyo anadokeza lazima wapambane mwanzo mwisho kukabili washindani wengine wanaokuja kwa kasi kwenye michuano ya muhula huu.

Kocha huyo anadokeza kuwa wachana nyavu wake wana kibarua kigumu kukabili wapinzani wao kama KSG Ogopa ambayo kufikia sasa imeketi kileleni mwa jedwali kwa kukusanya pointi 22, sita mbele Melta Kabiria sawa na WYSA United baada ya kila moja kupiga patashika nane. Anasisitiza kuwa hawana lingine ila lazima wachezaji wake watie bidii zaidi michezoni ili kufufua mtindo wa kushinda mechi zao.

”Kusema ukweli kujipigia debe ninaamini vijana wangu wana uwezo wa kufanya kweli. Wiki iliyopita tulishinda Melta Kibiria kwa mabao 2-0 matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi,” akasema.

Kocha huyo anasema kuwa ukosefu wa viwanja vya kutosha pia huchangia timu nyingi kutopata muda wa kushiriki mazoezi. ”Mfano sisi hufanyia mazoezi katika uwanja wa Kihumbu-ini Kangemi pia unatumiwa na timu zingine zaidi ya kumi. Itakuwa vizuri pia viongozi wa shule za msingi mitaani wafungue viwanja vyao kwa ajili ya kunoa makucha ya wachezaji wanaokuja.”

Katika mpango mzima klabu hiyo ni miongoni mwa vikosi nyingi vinavyozidi kukuza talanta za wanasoka wanaokuja mitaani ambapo mwanzilishi huyo anasema itakuwa fahari kuu kwake kuona amelea wachezaji na kufaulu kuteuliwa kuchezea timu ya Harambee Stars.

Klabu hiyo tangia ianzishwe 2007 inajivunia kushinda taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2018 ilipolaza Leeds United mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa goli 1-1.

Timu hiyo ilishinda ubingwa huo baada ya kulinyemelea kwa miaka huku ikiweka tumaini kuwa baada ya dhiki ni faraja.

Red Carpet FC imeundwa na wachezaji kama: Soita Brian, Isaac Sawanga, Ken Juma, Luiz Shanale, Cyrus Makali, John Kamau, Vitalis Owiti, Cetty Ligogo, Dominic Angaya, Erick Shivoko, Duke Abuya, Erick Ochieng, Geofrey Alma na Francis Mmani (nahodha na naibu wake) kati ya wengine.

Habari zinazohusiana na hii