• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Japan waponda Mongolia 14-0 katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2022

Japan waponda Mongolia 14-0 katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2022

Na MASHIRIKA

FOWADI Takumi Minamino wa Liverpool alifunga bao na kusaidia timu yake ya taifa ya Japan kupepeta Mongolia 14-0 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Minamino ambaye kwa sasa anachezea Southampton kwa mkopo, alifungulia Japan ukurasa wa mabao katika dakika ya 13 kabla ya Yuya Osako wa Werder Bremen nchini Ujerumani kucheka na nyavu mara tatu.

Wafungaji wengine wa magoli ya Japan walikuwa Daichi Kamada, Takuma Asano, Hidemasa Morita na Khash Erdene Tuyaa aliyejifunga.

Sho Inagaki, Junya Ito na Kyogo Furuhashi walifunga mabao mawili kila mmoja.

Ushindi huo wa Japan unamaanisha kwamba watafuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo 2022 kutoka bara Asia iwapo watapepeta Myanmar katika mchuano ujao utakaowakutanisha jijini Yokohama, Japan mnamo Juni 3, 2021.

Mechi kati ya Japan na Mongolia ilichezewa mjini Chiba, Japan kutokana na kanuni kali za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona katika nchi ya Mongolia inayoshikilia nafasi ya 190 kwa mujibu wa viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA).

Mnamo Machi 29, 2021, Canada walipokeza Cayman Islands kichapo cha 11-0 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Afrika Kusini, DR Congo na Angola kati ya vigogo wa soka...

Ubelgiji bila De Bruyne na Lukaku yakomoa Belarus 8-0