• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Aliyefutwa sababu ya ujauzito atuzwa Sh1.4m

Aliyefutwa sababu ya ujauzito atuzwa Sh1.4m

Na BRIAN OCHARO

MWANAMKE aliyefutwa kazi kwa kuwa mjamzito ana sababu ya kutabasamu baada ya mahakama ya Mombasa kuamuru alipwe fidia ya Sh1.4 milioni.

Jaji wa mahakama ya Viwanda, James Rika alibainisha kuwa mwanamke huyo alidhulumiwa kutokana na ujauzito wake. Kwamba Abson Motors Ltd ilishindwa kuthibitisha hakukuwa na ubaguzi.

“Inaweza kuhitimishwa tu kwamba dokezo hili la jumla, kuhusu huduma za mwanamke huyo kutohitajika tena lilikuwa kisingizio. Sababu ya msingi ni kwamba mwanamke huyo alikuwa mjamzito, na hakuwa mzima kiafya. Kuwa mjamzito, machoni mwa mshtakiwa hakukuwa na tija kazini. Na kwa hivyo anaweza kutolewa,” akasema Jaji Rika.

“Kutapika, kukosa usingizi na uchovu hakukuwa na mwisho. Mshtakiwa alimwona kama mzigo mkubwa katika biashara yake. Akaamua kumfuta akimwambia kwa ukali kwamba huduma zake hazihitajiki tena,” akaongeza.

Kufahamu

Stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani zilithibitisha kuwa kampuni hiyo ilifahamu kuwa mwanamke huyo alikuwa mjamzito na anaugua magonjwa yanayohusiana na ujauzito, kwa hivyo korti iliamua kuwa hakuna shaka kwamba kampuni hiyo ilijua kuwa alikuwa mjamzito.

“Zaidi ya ubaguzi wa ujauzito, ni wazi kuwa mshtakiwa hakuzingatia sheria alipokatiza mkataba wa mlalamishi. Hiyo ni kusema kwamba hata mdai angekuwa hajapata ujauzito, na aliambiwa tu kwamba huduma zake hazihitajiki tena, kufutwa bado kungekuwa dhaifu kihalali,” jaji alibaini.

Kwa hivyo korti imetangaza kuwa mwanamke huyo alibaguliwa kutokana na ujauzito wake na akampa malipo ya Sh1.4 milioni pamoja na mshahara wa mwezi mmoja ambao hajalipwa.

Mwanamke huyo aliyetambuliwa kama AKO alifanya kazi kama mpokeaji katika Abson Motors Ltd lakini alifutwa kazi mara tu alipoanza kupata magonjwa yanayohusiana na ujauzito.

Baada ya kuonyesha dalili ya ujauzito, mwanamke huyo alipewa siku chache za kupumzika nyumbani ambayo ilirekodiwa kama likizo ya kila mwaka lakini baada ya kurudi kazini alipewa barua ya kufutwa.

Kulingana naye, msimamizi mkuu wa kampuni hiyo kabla ya kumtuma nyumbani kwa likizo ya lazima alimsihi ajiuzulu kwa ahadi kwamba atalipwa mshahara wa miezi mitatu.

Hata hivyo alikataa na kusisitiza usawa wake na nia ya kuendelea kufanya kazi. Lakini kampuni hiyo ilimfuta kazi licha ya kusema kuwa angeendelea na kazi bila ya kutatizwa na ujauzito.

Baada ya tukio hili, mwanamke huyo alifungulia mashtaka kampuni hiyo kwa kumdhulumu kutokana na ujauzito wake.

Katika nyaraka zake za korti zilizowasilishwa mbele ya Jaji Rika, mwanamke huyo alilalamika kuwa barua ya kumfuta kazi haikuonyesha sababu za uamuzi huo.

“Sikuwasilishiwa mashtaka yoyote dhidi yangu wala kusikilizwa juu ya madai yoyote kabla ya uamuzi huo kuafikiwa,” alisimulia.

Kabla ya kufutwa, mwanamke huyo alidai kuwa menega wa kampuni hiyo Bw Simon Mwaniki alimsawishi aandike barua kuwa hangeweza kuendelea na kazi kwasababu ya ujauzito.

“Nilipokataa kutimiza hayo, nilifutwa bila kuambiwa makosa niliyofanya,” alisema.

Kampuni hiyo hata hivyo iliokubali kuwa mwanake huyo alikuwa ni mfanyikazi wake lakini ilikana kwamba alifutwa kwa ubaguzi wa ujauzito.

“Kampuni haikujua kuhusu ujauzito wake. Hakukuwa na ubaguzi wowote. Alipewa notisi ya kufutwa na kulipwa fedha zake. Hana haki ya kulipwa faida yoyote, ” kampuni hiyo ilisema.

Wakti huo huo, kampuni hiyo ilijitetea ikidai kwamba mlalamishi alifutwa kwa mujibu wa sheria. Pia , mshtakiwa ilimlaumu mwanamke huyo kwa kushindwa kuwaarifu wasimamizi wake kuhusu ujauzito wake na kutotoa stakabadhi za kuonyesha kuwa alikuwa mgonjwa na mjamzito.

“Alipewa msaada kamili wakati wa ujauzito wa kwanza, ni jambo lisilowezekana kwamba angebaguliwa wakati wa ujauzito wa pili. Alijiuzulu kwa hivyo hawezi kudai mkataba wake ulikatishwa, ”kampuni hiyo ilijitetea.

Hata hivyo, mahakama ilishikilia kuwa mwanamke huyo alidhulumiwa.

You can share this post!

ODM yadai viongozi 4 wamedandia handisheki kujifaidi

OMAUYA: Handisheki isigeuzwe kisa cha nyani na mbwa