• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
DINI: Hatuna budi kusali wakati wa mabaya na mazuri tusije tukatekwa na kiburi!

DINI: Hatuna budi kusali wakati wa mabaya na mazuri tusije tukatekwa na kiburi!

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

SALA inagema na kufungulia neema za Mungu. Kuna aliyesema hivi, “Lazima tusali wakati wa magumu na dhoruba, vinginevyo tutakosa imani na amani. Lazima tusali wakati wa mafanikio, vinginevyo tutakuwa na kiburi.

Lazima tusali wakati wa hatari, vinginevyo tutakuwa na woga na mashaka. Lazima tusali wakati kuna ulinzi, vinginevyo tutajiamini kupita kiasi tutaanguka.

Padre alimuuliza mtoto Jimmy: “Unasali sala zako za usiku, wewe mtoto mdogo?”Jimmy alijibu, “Ndiyo padre.” Padre alizidi kudadisi, “Na unazisali asubuhi?” Jimmy alijibu, “Hapana, Padre, asubuhi siogopi.”

Usisali tu wakati unaogopa. Sali hata kama kama unajihisi jasiri. Zaidi ya kusali Biblia yasema, “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote…” (1 Timetheo 2: 1-4).

Katika maneno “kwa ajili ya watu wote” na wewe jiombee. Matatizo yanayokupata ni asilimia kumi. Kuyapokea kwa dua, kwa shukrani ni asimilia tisini.

“Usisali kukwepa matatizo. Usisali kuwa na faraja katika hisia zako. Sali kufanya mapenzi ya Mungu katika kila hali” (Samuel M. Shoemaker). Kuna kusudi la Mungu katika kila tatizo.Unapoyakabili matatizo, yapokee kwa dua. Katika majaribu mfalme Daudi alisali, “Ee Bwana, uyasikie maombi yangu, uisikilize sauti ya dua zangu” (Zaburi 86:6).

Dua ni maombi yanayoelekezwa kwa Mungu. Umedhulumiwa? Yapokee kwa dua. Daudi alipokuwapo pangoni sababu ya kudhulumiwa alisali, “Kwa sauti yangu nitamlilia Bwana, kwa sauti yangu nitamwomba Bwana dua” (Zaburi ya 142: 1).Dua yako iwe dua chanya.

Yapokee kwa dua chanya si kama Eliya. “Eliya alijiombea roho yake afe…akasema ‘yatosha sasa,’ …malaika akamgusa akamwambia, “Inuka ule,” ( 1 MFalme 19:4-9).

Dua alikuwa na dua hasi. Mungu wetu ni Mungu wa walio hai.Yesu hakuja kuondoa baadhi ya mizigo bali kutupa mabega imara. Naye alikuwa na mzigo wa upendo.“Usisali kwa ajili ya mizigo miepesi zaidi bali kwa ajili ya mgongo wenye nguvu zaidi,” alisema Theodore Roosevelt. Omba Mungu aimarishe mabega yako.

Anaweza akakutua mzigo au akaimarisha mabega yako. Eliya badala ya kuomba afe, angeomba Mungu amwimarishe.Waombee wengine wayapokee matukio mabaya. Waombee wengine wabadilike. Kwenye meza ya upasuaji, alisimama daktari wa upasuaji na mtawa wa kike.

Walikuwa wamefanya kazi pamoja muda mrefu. Walivyowapasua wagonjwa daktari alimtazama mtawa na kumkejeli, “Katika upasuaji wote hatajaiona roho.”Mtawa alijibu, “Tutaiona roho yako kabla ya wewe kuaga dunia. Huwezi kutuponyoka ninakuombea.”

Daktari huyo alijibu kila mara, sala hizo mwekee mwingine ambaye ana uwezekano wa kwenda mbinguni. Alienda likizo na habari ilikuwa aliugua ghafla na kuaga dunia.

Mtawa alienda kanisani kusali. Alimwambia Mungu, “Naamini uliokoa roho yake kwa sala zangu. Unaweza kunihakikishia.” Mungu alimwambia kuwa alipelekwa hospitalini iliyokuwa inaendeshwa na watawa; yeye aliomba wamuite padre. Alibatizwa na kupokea mpako wa wagonjwa.

“Ukimwombea mwingine, utasaidiwa wewe” (Methali ya Kiyiddish). Waombee wengine na wewe upate baraka. Waombee wengine na wawe upate neema.“Wengi wetu tuna matatizo makubwa ya kusali tunapokuwa na matatizo madogo, lakini tuna matatizo madogo ya kusali tunapokuwa na matatizo makubwa” (Richard P. Cook).

Katika matatizo madogo sali, katika matatizo makubwa sali sana. Unaposalitiwa, Mungu anataka dua yako. Unapofiwa, Mungu anataka dua yako. Unapokuwa mgonjwa, Mungu anataka dua yako.

Mtoto wako anaposhindwa mitihani, Mungu anataka dua yako. Biashara yako inapojikongoja, Mungu anataka dua yako. Unapokuwa na figisufigisu na ndugu zako wa tumbo moja, Mungu anataka dua yako.

You can share this post!

Mwanasheria Mkuu kukata rufaa ya BBI katika Mahakama ya Juu

Rais Uhuru abadilisha mbinu kuendelea kung’ata Mlimani