• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:36 AM
FIDA yataka wawaniaji wenza wa urais, ugavana wawe wanawake

FIDA yataka wawaniaji wenza wa urais, ugavana wawe wanawake

NA BENSON MATHEKA

SHIRIKISHO la Mawakili Wanawake Kenya (FIDA-Kenya) linataka kila mwaniaji urais na ugavana mwanamume katika uchaguzi mkuu ujao kumteua mwaniaji mwenza mwanamke.

Chama hicho kinasema kila juhudi zinapaswa kufanywa kuhakikisha usawa wa jinsia umetimizwa katika nyadhifa za uongozi.

“Kwa wakati huu, wawaniaji wa viti vya kisiasa na miungano wanachagua manaibu wao na wawaniaji wenza kulingana na sheria na mwongozo wa IEBC. Mchakato huo unafaa kuzingatia usawa wa jinsia kwamba kuwe na naibu rais mwanamke kwa wagombeaji wote wa urais wanaume,” Mwenyekiti wa FIDA- Kenya, Nancy Ikinu alisema kwenye taarifa.

Kulingana na FIDA- Kenya, kuwa na naibu rais mwanamke kutaimarisha demokrasia nchini. Wanawake kadhaa akiwemo kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua, Gavana Charity Ngilu (Kitui), Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a, Sabina Chege, wanapigiwa upatu kuteuliwa mwaniaji mwenza wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga huku Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru (Kirinyaga) na Mbunge wa Kandara Alice Wahome wakipigiwa upatu kuteuliwa mgombeaji mwenza kwa Naibu Rais William Ruto.

“Vile vile, tunataka pale ambapo kuna mwaniaji ugavana mwanamume, lazima awe na mgombea mwenza mwanamke,” alisema Bi Ikinu.

Alisema FIDA Kenya inataka vyama vyote vya kisiasa, miungano, Tume ya Uchaguzi (IEBC), Jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa na Msajili wa vyama vya kisiasa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za kugombea viti vya uongozi.

“Tunaomba taasisi zote zinazosimamia na kusaidia mchakato wa uchaguzi kuhakikisha wanawake wanapata elimu kuhusu uchaguzi na jamii, kuwapa wagombeaji wanawake usaidizi kamili, mafunzo na pesa na kuondoa ubaguzi wa kisiasa unaozuia wanawake kushiriki kama wapigakura au wagombeaji,” alisema

  • Tags

You can share this post!

Magoha ataka usajili wa upesi wa watahiniwa

TAHARIRI: Usimamizi wa basari sharti urekebishwe

T L