• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
TAHARIRI: Usimamizi wa basari sharti urekebishwe

TAHARIRI: Usimamizi wa basari sharti urekebishwe

NA MHARIRI

KUUNGAMA kwa Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kwamba hazina za basari zinazosimamiwa na wanasiasa zimekolewa na ufisadi wakati wanafunzi wengi wanakabiliwa na tisho au wamekatiza masomo kwa kukosa karo, kunafaa kutumiwa kurekebisha hali hiyo.

Kukiwa na nia njema, ambayo inasikitisha ni vigumu kupatikana miongoni mwa viongozi wetu, mfumo wa basari unafaa kufanyiwa mageuzi ili kuhakikisha unafaidi watoto wanaolengwa.

Serikali ina uwezo wa kuanzisha mageuzi hayo iwapo anavyosisitiza waziri, ina nia njema ya kuhakikisha watoto wote wanaofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na kidato cha kwanza.

Katika juhudi za kuhakikisha ametimiza mpango wa serikali wa kuwapa watoto wote elimu ya msingi, Profesa Magoha ameagiza walimu wakuu kukubali wanafunzi wote hata kama hawana karo ya shule.

Hata hivyo, kuna maelfu ya watoto wanaoripotiwa kukosa hata nauli ya kuwafikisha shule walizoitwa kujiunga na kidato cha kwanza ilhali anasisitiza ni lazima kila mwanafunzi ajiunge na shule aliyoitwa.

Kumekuwa na ripoti za wachache wanaofanikiwa kusafiri mwendo mrefu kwa miguu kufika katika shule walizoitwa huku maelfu wakikwama kwa kukosa namna basari zinazonuiwa kuwafaidi zikiporwa au kunufaisha watoto wa matajiri.

Kwa heshima zote kwa waziri, msimamo huu wa kukataza wanafunzi kuhamia shule hasa zilizo karibu na ambazo wazazi wanaweza kumudu karo kulingana na uwezo wao, ni kukiuka haki ya mwanafunzi, sawa na wanavyofanya wanaowanyima basari na kupatia watoto wa matajiri walio na ushawishi.

Hivyo basi, iwapo serikali inaweza kuonyesha mfano mwema na kulegeza masharti ya kujiunga na kidato cha kwanza na kuanzisha mchakato wa sheria wa kuhakikisha hazina zote za basari zinasimamiwa kwa uwazi na uadilifu, ingekuwa inafanyia haki watoto werevu wanaotoka familia masikini katika nchi hii.

Wanasiasa na washirika wao wanaosimamia hazina hizo na kuvuruga haki kwa watoto walio na mahitaji kupata hela hizo wanapasa kulaaniwa.

Ni ukosefu wa hisia za binadamu kwa mtu ambaye amebarikiwa kuwa na pesa za kulipia mwanawe karo kukubali kupokea pesa hizo za basari, na hivyo kuwanyima mayatima na wale ambao wazazi wao hawajiwezi.

Hazina hizo zinafadhiliwa kwa pesa za umma kwa kutambua kuwa elimu ni mojawapo wa vitu ambavyo vinaweza kusaidia wasio na uwezo kujinasua.

Lakini kwa kuendelea kuwanyima haki hii ya basari, wahusika wanachangia katika kuendeleza umaskini na kurudisha jamhuri yetu nyuma.

You can share this post!

FIDA yataka wawaniaji wenza wa urais, ugavana wawe wanawake

Basari za NG-CDF zimejaa ufisadi, Magoha afichua

T L