• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Hasara kuu kongamano la magavana likifutiliwa mbali

Hasara kuu kongamano la magavana likifutiliwa mbali

Na PIUS MAUNDU

SHINIKIZO kuhusu kuwalipa wafanyabiashara waliokuwa wamepatiwa kandarasi za kuuza bidhaa na huduma katika kongamano la saba la ugatuzi zimeshika kasi.

Baraza la Magavana Alhamisi lilifutilia mbali kongamano la siku nne lililopangiwa kufanyika mjini Wote, Kaunti ya Makueni, kuanzia jana Jumatatu, likitaja kuongezeka kwa maambukizi ya Covid-19 na kuibua malalamishi kutoka kwa wafanyabiashara.

“Waandalizi wa kongamano hilo la ugatuzi wanapaswa kubuni haraka mbinu ya kuhakikisha kwamba wote waliokuwa wamepatiwa kandarasi za kuleta bidhaa na huduma wamelipwa,” alisema Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana.

Wito sawa na huo ulitolewa na wafanyabiashara kadhaa waliokuwa wanamezea mate faida ya mamilioni lakini badala yake wakapata hasara kuu.

Wafanyabiashara waliokuwa wamewasilisha mamia ya hema na viti vyenye thamani ya Sh100 milioni katika eneo ambapo kongamano hilo lingeandaliwa walikuwa bado wanabomoa kufikia Jumapili.

Jamii ya wafanyabiashara mjini Wote, ilikadiria hasara kuu hapo Jumatatu, siku ambayo walitarajiwa kupata kivuno kikuu.

Hatua ya kufutilia mbali hafla hiyo katika dakika ya mwisho ni pigo kuu kwa biashara eneo hilo na wafanyabiashara chipukizi wanaojishughulisha na bidhaa za chakula.

“Tulikuwa tayari tumenunua bidhaa za chakula zinazoharibika upesi kutoka Nairobi na kuandaa timu yetu ya kushughulikia maakuli wakati Baraza la Magavana lilipotangaza kufutiliwa mbali kwa kongamano hilo. Tutapata vipi hela zetu,” aliuliza Bi Christine Mutua, akifichua kwamba alikuwa amechukua mkopo kujitayarisha kwa kongamano hilo.

Bw David Masika, anayemiliki Kusyombunguo Hotels mjini Wote, ambapo idadi kubwa ya wajumbe walikuwa wamehifadhiwa malazi, alisema amepata hasara ya takriban Sh10milioni.

“Idadi kubwa ya wauzaji nyama ya ng’ombe, kuku, samaki na matunda tayari walikuwa wamewasilisha bidhaa. Ingawa ukarabati ghali tuliokuwa tumefanya utasalia, tutapata hasara ya chakula kwa sababu tulikuwa tumewafungia nje wateja wengine tukisubiri kushughulikia Baraza la Magavana,” alisema.

“Wafanyabiashara wote waliokuwa wamepatiwa kandarasi za chakula walikuwa wamekusanya vifaa ghali, vyakula na timu za kushughulikia vyakula wakati kongamano hilo lilipofutiliwa mbali. Tumepoteza takriban Sh30 milioni,” alisema Antony Ngunga, mwenyekiti wa muungano wa wafanyabiashara wa vyakula na hoteli eneo hilo.

Bw Ngunga na Bw Masika waliwataka wafanyabiashara walioathirika kukusanya orodha halisi ya bidhaa walizokuwa tayari wamewasilisha na kutaja kiasi halisi cha pesa walizotarajia kupata ili kusaidia katika shughuli ya kudai malipo kutoka kwa waandalizi wa kongamano hilo.

You can share this post!

Basari: Magoha asuta wabunge kwa ubaguzi

Taliban wawapa wanajeshi wa Amerika siku 7 waondoke