• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Hofu mkataba wa Kenya na Uingereza kuruhusu biashara huru ya bidhaa za kilimo kukachangia ongezeko la zile bandia mikakati isipowekwa

Hofu mkataba wa Kenya na Uingereza kuruhusu biashara huru ya bidhaa za kilimo kukachangia ongezeko la zile bandia mikakati isipowekwa

Na SAMMY WAWERU

BAADHI ya wakulima na mashirika yasiyo ya kiserikali yameibua wasiwasi kuhusu mkataba wa Kenya na Uingereza kuruhusu biashara huru ya mazao na bidhaa za kilimo, kati ya mataifa haya mawili.

Serikali ya Kenya na Uingereza zilifanya mazungumzo ya makubaliano mwaka uliopita, Kenya ikayaidhinisha Machi 2021.

Aidha, serikali pia iliwasilisha mkataba huo kwa Katibu Mkuu wa Jamii Muungano wa Afrika Mashariki (EAC).

Wakulima na wadauhusika katika sekta ya kilimo wanateta hawafahamu haliyomo kwenye mkataba huo, licha ya serikali kuupitisha.

“Umma haukushirikishwa kutoa maoni, hatujui yaliyomo,” akasema Bw Davies Nyachieng’a, afisa kitengo cha biashara na uwekezaji Shirika la Eco-News Africa, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Shirika hilo lisilo la kiserikali linalalamikia wananchi, hususan wakulima na wafanyabiashara kuwekwa gizani, katika mkataba huo muhimu na unaowahusu.

“Uingereza ilihamasisha wananchi wake kuhusu mkataba huo wa kibiashara. Kenya haikufanya hivyo, ni nini hicho serikali inaficha?” Bw Nyachieng’a akahoji.

Aidha, mkataba huo unalenga kuruhusu Kenya na Uingereza kuwa na biashara huru ya bidhaa na mazao ya kilimo, kati ya bidhaa nyinginezo.

Wakulima wanahofia ukianza kutekelezwa, huenda ukaathiri soko la bidhaa za kilimo nchini.

“Uingereza hupiga jeki wakulima wake kwa kuwanunulia pembejeo; mbolea, mbegu na dawa. Kenya, mikakati kama hiyo haipo. Mazao ya Uingereza yatasheheni nchini, yatakuwa ya bei ya chini, hivyo basi yetu yatakosa soko,” Caroline Kiragu, mkulima, akaambia Taifa Leo.

Wakulima na wadauhusika wanasema endapo yaliyomo kwenye mkataba huo hayatawekwa paruwanja, huenda jukwaa la uendeshaji biashara ya kimagendo likaundwa, wafanyabiashara matapeli wakitumia mwanya huo kuisakata.

  • Tags

You can share this post!

Lionel Messi sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na...

Leon Goretzka na Declan Rice kati ya wanasoka 5 wanaoviziwa...