• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Hofu wezi wakijaribu kufukua mwili wa mbunge

Hofu wezi wakijaribu kufukua mwili wa mbunge

Na CHARLES WANYORO

KULIZUKA sintofahamu katika kijiji cha Kaguma, Kaunti ya Meru baada ya wezi kuvamia kaburi la aliyekuwa mbunge wa Imenti ya Kati marehemu Gideon Mwiti wakitaka kufukua mwili wake na kuiba vito vya thamani (blingbling).

Polisi waliitwa haraka kuokoa hali baada ya genge hilo kufika katika kaburi hilo saa saba usiku wa kuamkia Jumapili, tukio ambalo liliwashangaza wanakijiji mno.

Japo idadi yao haikujulikana, wezi hao walitoroka baada ya vijana waliokuwa wakilinda kaburi hilo kuwaona na kupiga kelele wakiitisha msaada wa kupambana nao.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF), Frank Muthuri ambaye alikuwa rafiki wa marehemu, alisema aliamshwa usingizini baada ya kupokea simu ya vijana walinzi waliodai kuwa walikuwa wamepigwa kwa mawe.

Mmoja kati ya vijana hao alinyunyiziwa kemikali isiyojulikana iliyomwaacha akiwa hajitambui na kulazimika kubebwa juu ili kusaidiwa. Bw Muthuri alisema alikisia kuwa kaburi hilo lingevutia wezi baada ya kaburi la mtu mwingine mashuhuri kufukuliwa mnamo Juni katika eneo la Kiagu.

Bw Mwiti alihudumu kama mbunge kati ya 2013-2017 japo alianzisha miradi ya uwekezaji ambayo iliporomoka na mamilioni ya pesa za wanachama. Kaburi lake lilikuwa la kina cha futi nne pekee ikizingatiwa kuwa eneo hilo limejaa mawe na lilifunikwa kwa mchanga.

“Tulijua kuwa kaburi hilo lingevamiwa kutokana na kisa cha hapo awali. Hiyo ndiyo maana tuliwapa vijana wanne kibarua cha kutoa ulinzi ila wakatupigia simu wakisema walivamiwa na genge lililowarushia mawe,”

“Walisema kuwa wanahofia usalama wao na hawataendelea kulilinda. Lazima usalama uimarishwe la sivyo kaburi la mheshimiwa litafukuliwa,” akasema Bw Muthuri.

Hata hivyo, polisi katika kituo cha polisi cha Kaguma walifika na kutoa ulinzi japo kaburi hilo halikuwa limeguswa. Bw Muthuri alishuku madai ya vijana hao, akisema huenda ilikuwa njama ya kutaka walipwe ujira wa Sh1,000 badala ya Sh500.

Kulingana na Bi Isabella Mugure ambaye ni mfanyakazi anayehusika na kuangazia maslahi ya watoto mayatima eneo hilo, huenda wezi hao walivutiwa na makazi ya kifahari ya marehemu na kuchochewa na mahubiri ya askofu aliyeongoza mazishi ya mwanasiasa huyo.

“Mhubiri alisimulia jinsi mwili wa tajiri aliyezikwa kwa jeneza la bei ghali na nguo na viatu vya bei ghali ulifukuliwa. Waliona jeneza la mheshimiwa lilikuwa ghali na walifikiria alizikwa na vito vya thamani,” akaongeza.

You can share this post!

Gavana Kingi apinduliwa ODM kwa ‘kuasi’ Raila

Wabunge wa maeneo kame wataka NG-CDF zaidi