• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Kenya imechanja tena wanamichezo 2,000 na wanaotangamana –Waziri Amina

Kenya imechanja tena wanamichezo 2,000 na wanaotangamana –Waziri Amina

Na GEOFFREY ANENE

WIZARA ya Michezo imefichua kuwa wanamichezo 2,000 wamepokea chanjo ya pili juma hili ya ugonjwa wa covid-19 kupitia kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS).

Idadi hiyo pia inajumuisha watu wanaotangamana sana na wanamichezo, ambao ni maafisa wa timu hizo, na maafisa kutoka kwa wizara hizo.Waziri wa Michezo Amina Mohamed alisema kuwa zoezi lililokamilika

Ijumaa lililenga timu zinazojiandaa kushiriki Olimpiki mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 na Olimpiki ya Walemavu mnamo Agosti 24 hadi Septemba 5 mjini Tokyo, Japan.

Timu hizo ni Shujaa na Lionesses, ambazo timu za taifa za raga ya wachezaji saba kila upande za wanaume na wanawake mtawalia, Malkia Strikers (voliboli ya kinadada), wanariadha, kikosi cha Olimpiki ya Walemavu, ulengaji shabaha kwa kutumia bunduki, judo na taekwondo.

“Chanjo hiyo pia ilipeanwa kwa timu za taifa zinazojiandaa kwa mashindano ya Afrika ama Dunia zikiwemo Kabaddi, Harambee Starlets, Harambee Stars na mpira wa vikapu. Wafanyakazi wa Mbio za Magari za Dunia za Safari Rally pia walichanjwa,” alisema waziri huyo.

Klabu 11 zinazoshiriki Ligi Kuu ya soka nchini kutoka kaunti ya Nairobi pia zilipokea chanjo hiyo ya AstraZeneca. Timu hizo ni Wazito, Bidco United, Gor Mahia, Kariobangi Sharks, KCB, Mathare United, Nairobi City Stars, Posta Rangers, Sofapaka, Tusker na AFC Leopards.

Wizara ya Michezo ilishukuru Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na NMS kwa kuwasilisha chanjo hizo na usaidizi kwa timu zinazojiandaa kushiriki michezo.Pia, ilishukuru serikali za kaunti za Mombasa, Uasin Gishu na Elgeyo Marakwet kwa kuhusika katika chanjo ya wanamichezo wanaoishi nje ya Nairobi.

“Ningependa kuhakikishia wanamichezo wote waliopata chanjo ya kwanza kuwa Wizara itahakikisha wanapokea chanjo ya pili mara tu dozi hizo zitapatikana,” alisema Mohamed.Alifichua kuwa wanafurahi kuwa wanamichezo waliochanjwa mara ya kwanza ndani na nje ya Kenya katika siku 30 zilizopita, hawajapatikana na virusi vya corona.

“Tuna matumaini makubwa kuwa hakutakuwepo na visa vya maambukizi tunapojiandaa kwa mashindano ya Olimpiki, mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, Safari Rally, Riadha za Dunia za Under-20 na mashindano mengine ya kimataifa.”

  • Tags

You can share this post!

Kenya imechanja tena wanamichezo 2,000 na wanaotangamana...

Mtandao wa ‘Ardhi Sasa’ utaweza kuzima matapeli wa...