• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 12:25 PM
MARY WANGARI: Kongamano la UN litumiwe kuimarisha mifumo ya uzalishaji lishe

MARY WANGARI: Kongamano la UN litumiwe kuimarisha mifumo ya uzalishaji lishe

Na MARY WANGARI

UMOJA wa Mataifa (UN) umeonya serikali za dunia kuwa majanga yanayozidi kuchipuka kila uchao yataendelea kushuhudiwa iwapo mikakati thabiti ya kukabiliana na kiini cha matatizo hayo haitabuniwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo la kimatiafa, kila wakati majanga yanapotokea, viongozi wa mataifa wamekuwa wakijishughulisha na suala la “nini” kilitendeka na kupuuza “ni kwa nini” kilitendeka.

Shirika hilo limeashiria hofu kuwa matatizo hayo kama vile mafuriko, maporomoko ya ardhi, ukame na njaa, mikurupuko ya maradhi, mioto nyikani na kadhalika, yatazidi kushuhudiwa iwapo mikakati jumuishi ya kudhibiti majanga hayo haitabuniwa.

Kauli yake imejiri wakati mwafaka baada ya hatua ya Rais Kenyatta wiki jana kutangaza ukame unaohangaisha wananchi Kaskazini ya Kenya kuwa janga la kitaifa.

Tangazo hilo lilijiri wakati kaunti 12 miongoni mwa 23 katika maeneo kame, tayari zinaathiriwa na makali ya ukame na ukosefu wa chakula.

Kwa miongo mingi, wadau katika sekta ya kilimo hawajakuwa wakitilia maanani michakato muhimu inayohusika wakati wakulima wanapoenda shambani na chakula kinapowafikia watu mezani.

Kuanzia upanzi wa mbegu za kiwango cha juu, vifaa bora vya kilimo, mifumo kabambe ya kuvuna na kuhifadhi mazao na usafirishaji ni baadhi tu ya masuala muhimu yanayohusika kuhakikisha kuwepo kwa chakula cha kutosha nchini.

Mbali na hayo, kuna suala nyeti kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa kujiepusha na ukataji miti kiholela na kuvuruga chemchemi za maji ili kuzuia athari hasi za mabadiliko ya hali ya hewa.

Inavunja moyo kuwa licha ya maendeleo katika Sayansi na Teknolojia, Kenya hupoteza kiwango kikubwa cha mazao kutokana na mbinu duni za kuvuna na kuhifadhi mazao.

Mahangaiko

Si ajabu basi kwamba mwaka baada ya mwaka huwa tunashuhudia mamia ya raia wakihangaishwa na ukame hasa wakati ulimwengu unagubikwa na mabadiliko ya anga.Matokeo yake ni utapiamlo hasa miongoni mwa watoto na vita baina ya jamii za wafugaji na wakulima kung’ang’ania raslimali chache zilizosalia za malisho na maji.

Serikali imejitahidi kutimiza Ajenda Nne Kuu kuhusu Ruwaza 2030, mojawapo ikiwa kuhakikisha kuwepo kwa Chakula na Lishe ya Kutosha kwa Wakenya wote.Ili kufanikisha maazimio hayo, mikakati madhubuti inahitajika kubuniwa kwa dharura kuimarisha mifumo ya uzalishaji chakula.

Kongamano Kuu la UN kuhusu Mifumo cha Chakula Duniani litakaloandaliwa Septemba 23, litakuwa fursa kwa wadau kujadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya chakula nchini.

[email protected]

You can share this post!

Ukweli kuhusu chanjo za corona zilizoruhusiwa nchini

CECIL ODONGO: Kupe wa kisiasa wataponza Mudavadi na Kalonzo...