• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mhukumiwa aeleza jinsi walivyomuua naibu gavana

Mhukumiwa aeleza jinsi walivyomuua naibu gavana

Na BRIAN OCHARO

MHUKUMIWA katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Kenneth Kamto, ameeleza jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa.

Marehemu alipigwa risasi nyumbani kwake mtaa wa Nyali, Kaunti ya Mombasa mnamo Desemba 12, 2018 wakati watu wasiopungua watatu walimvamia.

Imefichuka kuwa, washambuliaji walichunguza nyumba kadhaa za kifahari katika eneo hilo kati ya Desemba 10 na 11, kabla ya kuvamia siku iliyofuata.

Muasya Kiteme almaarufu kama ‘Mwaa’, ambaye alikubali kuwa shahidi katika kesi hiyo, amedai kuwa wizi huo ulipangwa mnamo Desemba 10 na kutekelezwa siku mbili baadaye.

Anatumikia kifungo cha miaka 15 jela baada ya kuingia katika makubaliano na upande wa mashtaka awe shahidi.

Kulingana naye, alipokea simu asubuhi Desemba 10, kutoka kwa rafiki yake wakakubaliana kukutana katika eneo la Sosiani, Kongowea. Rafiki yake alifika akiandamana na mwingine.

“Aliniambia kuwa kuna kazi ambayo inahitajika kufanywa siku hiyo,” alisema.

Walikutana tena saa moja usiku wakapanga namna wangevunja nyumba Nyali na kuiba mali.

Mpango wao kuiba uligonga mwamba siku hiyo, wakakutana tena saa moja usiku uliofuata (Desemba 11).

“Tulikaa mahali hapo karibu hadi saa saba usiku. Dakika chache baadaye, tuliruka juu ya uzio wa nyumba na kuingia katika boma moja hapo. Wakati huu niligundua mmoja wetu alikuwa na bastola,” alisema.

Walifunga mikono ya mlinzi wa nyumba hiyo kwa kamba ya mkonge lakini hawakufanikiwa kuingia ndani kwa sababu ya ving’ora vya usalama.

Alieleza kuwa, walipoondoka kurudi nyumbani, walimwona Bw Kamto akiegesha gari lake.

Nyumba ya marehemu haikuwa mbali na ile ya kwanza waliyovamia, kwa hivyo walikimbia na kupanda ukuta na kuingia kwa mwendazake.

“Tulikaa kumsubiri Bw Kamto, ambaye alikuwa kwenye simu,” alisema.

Rekodi za korti zinaonyesha kwamba marehemu alitumia takriban dakika 10 nje ya nyumba yake akizungumza kwa simu.

Alipokuwa akiingia ndani ya nyumba yake, kutoka mlango wa nyuma, alisema walimfuata lakini walipofika mlangoni, walikutana naye akirudi nje ndipo makabiliano yakaanza.

“Taa zilikuwa zimewashwa kwa hivyo sote tulijifunika nyuso. Tulimshambulia na kupekua nyumba,” alisema, na kuongeza kuwa waliondoka na vitu vichache ambavyo walikuwa wameiba.

Baada ya tukio hilo, Bw Kiteme alipanda gari na kutorokea Mwingi lakini alikamatwa baada ya miezi mitatu ya uchunguzi.

Bw Kiteme alishtakiwa pamoja na Bw Gitonga na Bw Joseph Amwayi Mukabana.

Walituhumiwa kumpiga risasi Bw Kamto na kumuibia vitu vyenye thamani ya Sh28,000.

Mshukiwa mwingine katika kesi hiyo ni Bi Florence Mwanza ambaye ameshtakiwa pamoja na Bw Gitonga kwamba mnamo Januari 6, 2019, katika eneo la Kwa Bolu huko Kisauni, walipatikana na simu tatu za Bw Kamto na mkewe, Bi Fawzia Ndugu Omar.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 8 na 9.

You can share this post!

TSC yashtakiwa kukata ada walimu wasio vyamani

Hofu kuhusu waliko watu watatu baada ya boti kusombwa na...