• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Mswada unaolenga kudhibiti ulanguzi wa mihadarati wapitishwa na wabunge

Mswada unaolenga kudhibiti ulanguzi wa mihadarati wapitishwa na wabunge

Na CHARLES WASONGA

WALANGUZI wa mihadarati watakaopatikana na zaidi ya gramu 100 ya dawa hizo watatozwa faini ya Sh50 milioni au kutumikia kifungo cha miaka 50 gerezani au adhabu zote mbili kulingana na mswada mpya uliopitishwa bungeni Jumatano.

Mswada huo wa marekebisho ya sheria kuhusu udhibiti wa matumizi wa dawa za kulevya – Narcotics, Drugs and Psychotropic Substance Control Amendment Bill, 2020 – unalenga kuzima kabisa biashara ya mihadarati ambayo imekithiri nchini.

Wabunge waliupitisha mswada huo kwa kauli moja.

Kulingana na mswada huo ambao sasa unasubiri kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta kuwa sheria, wabunge pia waliweka kipengele ambacho kinasema kuwa watu watakaopatikana na mihadarati yenye uzani wa kuanzia gramu moja hadi 100 watatozwa faini ya Sh30 milioni au wafungwe gerezani kwa miaka 30 au adhabu zote mbili.

Vile vile, mtu yeyote ambaye atashtakiwa kwa kosa la kulangua mihadarati atazuiwa kuwania viti vya umma vya kuchaguliwa na kuteuliwa kwa miaka 30 baada ya kutumikia kifungo cha gerezani.

“Mtu ambaye atapatikana na hatia chini ya sheria hii atazimwa kuwania viti vya umma. Vile vile, walio hatiani hawatahitimu kuteuliwa kwa nyadhifa za umma kwa miaka 30 baada ya kutoka gerezani,” ikasema mswada huo uliodhaminiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Limuru Peter Mwathi.

Akiunga mkono mswada huo, Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema sheria hiyo pia itawanyima washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati dhamana ambayo wao hutoa kwa haraka wanapokamatwa.

“Hii ni yenye furaha kuu maishani mwangu. Hii ni kwa sababu kando na kulipa faini mara tatu ya thamani ya dawa hizo, walanguzi hawa sasa watafungwa kwa nusu karne. Hii ni sawa na kifungo cha maisha,” akasema.

Mswada huo pia unapendekeza adhabu kali kwa maafisa wa usalama ambao watasaidia ufanikishaji wa makosa chini ya sheria hii.

Kulingana na mswada huo, afisa wa usalama au wa umma ambaye atasaidia utekelezaji wa uhalifu wowote chini ya sheria kama vile kumficha mshukiwa au habari itakayosaidia kukamatwa kwa mshukiwa, watatozwa faini isiyozidi Sh20 milioni. Vile vile, afisa kama huyo anaweza kusukumwa gerezani kwa miaka 20.

Sheria hiyo pia inalenga kulazimisha wenye nyumba za makazi na wamiliki wa majumba ya kibiashara kuhakikisha kuwa wakodisha wa nyumba hizo hawazigeuzi kuwa ngome za kuuzia mihadarati.

“Kila mmiliki wa nyumba za makazi au za kibiashara wanahitajika kuweka sajili ya wapangaji wote katika nyumba hizo,” unasema mswada huo.

Baadhi ya kemikali ambazo hutumika kutengeneza dawa za kulevya ambazo hazikujumuishwa katika sheria kuu, zimejumuishwa katika mswada huu.

You can share this post!

Kaunti yasifu basari kwa kuboresha elimu

Walinzi wa rais wamnyaka mwanamume akinyemelea jukwaani Lamu