• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Ngatia atenga uhusiano wake na Rais akisaka kazi

Ngatia atenga uhusiano wake na Rais akisaka kazi

Na RICHARD MUNGUTI

HOFU kuwa mwaniaji wa wadhifa wa Jaji Mkuu, Bw Fred Ngatia, atapendelewa kwa kuwa alimwakilisha Rais Uhuru Kenyatta katika kesi za uchaguzi mkuu 2013 na 2017, ziliibuliwa Jumanne wakati wa mahojiano.

Makamishna wa tume ya kuajiri watumishi katika idara ya mahakama (JSC), walimweleza Bw Ngatia kwamba “Wakenya wamedai watapoteza imani na idara ya mahakama iwapo utateuliwa kuwa Jaji Mkuu.”

Wakimhoji Bw Ngatia, makamishna wa JSC, walimweleza kuwa mashirika mbali mbali na watu binafsi wamepeleka malalamishi wakielezea hofu yao kuhusu uteuzi wake kama Jaji Mkuu kumrithi Bw David Maraga.

Makamishna Jaji Mohammed Warsame, Jaji David Majanja na Everlyn Olwande, walimweleza Bw Ngatia, “Endapo hii tume itakuteua kuwa Jaji Mkuu Wakenya wataona kwamba tunakutuza kwa vile ulimtetea Rais Kenyatta katika kesi za kupinga ushindi wake katika chaguzi kuu za 2013 na 2017.”

Makamishna hao walimweleza Bw Ngatia kuwa ijapokuwa mchango wake katika kustawisha sheria ni mkubwa “bado wataona ametuzwa kwa kumtetea Rais Kenyatta katika kesi za uchaguzi zilizowasilishwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.”

“Utani umekuwa ukisheheni katika mitandao ya kijamii kwamba endapo unahitaji kumfahamu Jaji Mkuu mpya vuta kadi na jina la Fred Ngatia litajitokeza,” Bi Olwande alimweleza mwaniaji huyo.

Lakini akijibu malalamishi hayo, Bw Ngatia aliwahakikishia Wakenya kwamba “yeye ni mfuasi sugu wa sheria na haki na kamwe hawapaswi kubabaika.”

“Wakenya hawapaswi kuwa na wasiwasi wowote kwa vile mimi ni mtu wa kufuata sheria na haki,” Bw Ngatia alijibu JSC.

Pia alieleza kuwa kumwakilisha Rais Kenyatta si makosa kwa vile “ni Mkenya kama watu wengine na anastahili kuwakilishwa akishtakiwa.”

“Baada ya kukamilishwa kwa kesi hizo sijawahi kuwasiliana na Rais Kenyatta nikiomba uteuzi.”

Bw Ngatia alisema amewasilisha kesi nyingi dhidi ya Serikali kama ile ya kupinga adhabu ya kifo aliyosema imepata sifa kote ulimwenguni.

You can share this post!

Malalamiko ya MCK kwa DCI

Joho akariri Umoja wa Pwani ungalipo