• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 6:55 AM
Ni muhimu watu wapate chanjo ya corona – Dkt Kantaria ashauri

Ni muhimu watu wapate chanjo ya corona – Dkt Kantaria ashauri

Na SAMMY WAWERU

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya pembejeo ya Elgon Kenya, Dkt Bimal Kantaria amehimiza wananchi kujitokeza kupata chanjo ya virusi vya Corona.

Dkt Kantaria amesema chanjo hiyo ni muhimu, hasa kutokana na manufaa yake kusaidia kuzima makali ya Covid-19. Alisema hayo katika hafla ya ukumbusho wa Mwenyekiti wa kampuni hiyo yenye makao yake makuu Mombasa Road, jijini Nairobi, Bw Rajni Kantaria aliyeaga dunia Agosti 31, 2021.

Akihimiza wananchi kutilia maanani mikakati na kanuni kuzuia kuenea kwa Homa ya Corona, Dkt Kantaria alisema taifa na ulimwengu utaweza kukabili janga hili la kimataifa endapo watu watashirikiana.

“Covid ni hatari. Miezi kadha iliyopita niliugua,” afisa huyo akadokeza. “Mzee (akimaanisha Marehemu Rajni Kantaria) kabla kuaga dunia alikuwa amepata chanjo. “Mamangu pia aliipokea.

Sote tulikuwa tumeugua na kwa sababu ya chanjo tuliyopata, tulikuwa salama,” Dkt Kantaria akafichua.Mzee Rajni ndiye babake Mkurugenzi huyo, na anakumbukwa kutokana na jitihada na mchango wake kusaidia kuboresha sekta ya kilimo nchini.

Kutoka kulia, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya pembejeo ya Elgon Kenya, Dkt Bimal Kantaria, dadake, Bi Leena Kantaria na nduguye ambaye pia Mkurugenzi Mkuu mwenza Bw Baiju Kantaria wakati wa hafla ya ukumbusho wa Mwenyekiti wa kampuni hiyo Mzee Rajni Kantaria aliyefariki Agosti 31, 2021…PICHA/ SAMMY WAWERU

“Nashauri kila mmoja, na pia katika kampuni hii, hususan wazee kuhakikisha wamepata chanjo ya corona,” Dkt Kantaria akasema.Licha ya himizo watu wajitokeze kwa wingi kupata chanjo, wanasiasa wanaendelea kuandaa hafla za umma wengi wa wanaohudhuria wakionekana kutojali sheria na mikakati iliyopendekezwa kukinga kuambukizwa.

“Ugonjwa huu upo nasi na tutaishi nao kwa sababu tiba haijapatikana. Chanjo ni muhimu sana,” akasisitiza Dkt Kantaria. Kauli ya Dkt Kantaria imejiri wakati ambapo serikali inaendelea kutoa chanjo ya corona na kutaka wale ambao hawajajitokeza kufanya hima.

Wizara ya Afya inalenga watu milioni 10 kufikia Desemba 2021. Baadhi ya wananchi wanasusia chanjo, wakidai si salama, tetesi ambazo serikali kupitia Wizara ya Afya imetupilia mbali.

Kenya inasambaza dozi za chanjo ya AstraZeneca, Johnson & Johnson, Moderna, Pfizer na Sinopharm, ambazo zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani ndilo WHO.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens yapigwa fainali ya FKF Cup kuambulia patupu...

Man-United wakabwa koo na Everton ligini