• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Raila anavyosuka ODM na Nyanza tayari kwa 2022

Raila anavyosuka ODM na Nyanza tayari kwa 2022

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, ameanza kupanga chama chake na ngome yake ya kisiasa ya Nyanza huku akijiandaa kuzindua rasmi kampeni yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga amechukua hatua za kuhakikisha himaya yake ya kisiasa ya Nyanza inayohusisha kaunti sita za Kisumu, Siaya, Homa Bay, Migori, Kisii na Nyamira, imeungana kabla ya kutangaza rasmi azma yake ya kugombea urais kwa mara ya tano na muungano mpya wa kisiasa.

Chama chake pia kimeanza uchaguzi wa mashinani maeneo tofauti nchini na kukaribisha wanachama waliokiasi warudi.

Mnamo Ijumaa, Bw Odinga ambaye kufikia sasa hajatangaza rasmi azma yake, alipatanisha viongozi wa Kaunti ya Kisii na waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i, katika hatua ya kuhakikisha ngome yake ni thabiti.

Dkt Matiang’i alitofautiana na Gavana James Ongwae, Mwakilishi wa wanawake Janet Ong’era na Seneta Sam Ongeri, wakati wa uchaguzi mdogo wa eneobunge la Bonchari, ambao ODM ilishinda.

Viongozi hao walimlaumu Dkt Matiangi kwa kutumia polisi na maafisa wa utawala kuwahangaisha kwenye uchaguzi huo. Baada ya uchaguzi huo, Bw Odinga alikashifu matumizi ya polisi kwenye uchaguzi na kulaumu baadhi ya maafisa wa serikali kwa kuingilia masuala ya siasa na kuvuruga demokrasia.

Duru zinasema Bw Odinga alichukua hatua ya kuwapatanisha viongozi wa Kisii kuhakikisha ngome yake iko thabiti na kuzuia upenyo wa Naibu Rais William Ruto ambaye ana washirika kadhaa eneo hilo.

“Raila anafahamu kuwa katika ngome yake ya Nyanza, ni kaunti za Kisii na Nyamira pekee ambako Dkt Ruto anaweza kupenya kwa urais na kumpa ushindani. Hii ndiyo sababu ameamua kupatanisha Dkt Matiang’i na viongozi waliotofautiana,” asema mdadisi wa siasa, Bw Tom Maosa.

Anasema katika kaunti nyingine nne za Luo Nyanza, umaarufu wa Bw Odinga hauwezi kutikisika.

Wadadisi wa siasa wanasema kwa kuwa na kaunti sita za Nyanza nyuma yake, Bw Odinga atakuwa amejihakikishia kura zaidi ya 2.2 milioni. Kaunti za Kisii na Nyamira zina zaidi ya wapigakura 855,000 kulingana na sajili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya 2017. Kaunti nne za Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori zina jumla ya kura 1, 464,671 kulingana na sajili hiyo.

Kulingana na Bw Maosa, kwa kuunganisha eneo pana la Nyanza nyuma yake, Bw Odinga atakuwa ameongeza nafasi yake kujadili miungano na vigogo wa kisiasa wa maeneo mengine.

Ili kuhakikisha kwamba chama chake kitakuwa na nguvu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Odinga ameagiza mfumo wa uteuzi huru ambao hautaingiliwa na viongozi wa chama.

Hatua hii inanuiwa kuepuka wanaoshindwa kwenye mchujo kulalamika na kuhamia vyama vingine.

Chama hicho kiliondoa ada za usajili kwa wafuasi wanaotaka kuwa wanachama kama njia moja ya kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu ujao na ndicho chama cha pekee kinachoendelea na uchaguzi wa mashinani.

Bodi ya Taifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho, inayoongozwa na Bi Catherine Muma, imesema tangu iondoe ada hizom wanachama wapya 200,000 wamejiunga na ODM.

Mnamo Jumatano, Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna alisema kwamba uchaguzi umeanza katika kaunti za mashariki mwa nchi.

“Tunaendelea na uchaguzi wa mashinani. Tunajipanga,” alisema Bw Sifuna baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho jijini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Dressel aweka rekodi mpya kwenye uogeleaji wa 100m butterfly

Covid: WHO yaelezea hofu ya virusi vipya vya Delta