• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Samia azamia lugha yenye ladha ya kipekee

Samia azamia lugha yenye ladha ya kipekee

Na LEONARD ONYANGO

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Jumatano aliwachangamsha wabunge kwa lugha yenye ‘mahanjam’ alipokuwa akiwahutubia.

Alipokuwa akizungumzia uhusiano wa muda mrefu baina ya Kenya na Tanzania, Rais Suluhu alisema kuwa mataifa hayo mawili “yameunganishwa na mafundo matatu; ukaribu wa kijogorafia, udugu na historia”.

Rais Suluhu aliongeza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Kenya si wa hiari, bali ni wa lazima.

“Tuna ekolojia moja, tuna mipaka ya baharini na ardhini. Ndiyo kusema kuwa hata wanyamapori wetu ni ndugu na ni majirani. Kuna wale wanyamapori (kongoni) wanaokuja kupata mimba Maasai Mara Kenya na wanazalia Serengeti Tanzania. Ingekuwa wanyama hao wana uraia wangekuwa raia wa wapi?”

Alipokuwa akielezea kwa nini alifanya ziara yake ya kwanza rasmi nchini Kenya, Rais Suluhu alisema kuwa ‘mpangaji mwenye busara huanza kwa kufahamiana na majirani’.

“Busara inasema ukiwa mpangaji mpya lazima ujitambulishe kwa majirani. Kwa sababu mimi nilichukua hatamu za uongozi wa Tanzania hivi karibuni nimeona nije kwa majirani. Nimeanza na jirani wa Kenya ambaye ni jirani ndugu; nilipata mialiko mingi lakini nikasema nianze hapa, kwa sababu ya umuhimu na nafasi ya Kenya kwa Tanzania,” akasema.

Rais Suluhu pia alisema kuwa kafyu ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku ilizuia baadhi ya watu alioandamana nao kwenda kula nyama choma usiku.

“Nimebaini kuwa sehemu kubwa ya ujumbe nilioambatana nao wanajua vichochoro vya Nairobi. Wanajua nyama choma inapatikana wapi. Lakini kutokana na corona hawakuweza kujibamba. Nina wasiwasi tusije tukawabakisha nyuma,” akasema Rais Suluhu.

Kiongozi huyo wa Tanzania pia alitania wabunge na maseneta kuhusu namna wanatumia Kiswahili wakati wa mijadala Bungeni.

“Tulifurahishwa zaidi na uamuzi wenu wa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili Bungeni. Na-enjoy Kiswahili chenu kwani kina vionjo vingi,” akasema.

Alipohitimisha hotuba yake Rais Suluhu alisema: “Sisemi kwamba ninamalizia hotuba yangu, bali mniruhusu niathirishe maneno yangu hapa. Sijamaliza hotuba yangu kwa sababu tutasema maneno mengi katika majukwaa mengine tutakayokutana.”

“Tunapokutana Watanzania na Wakenya tunasema maneno mengi sana ya kuzungumza hayaishi; utani humo humo na vijembe humo humo; ndiyo mambo yanayochangamsha uhusiano wetu,” akasema.

You can share this post!

Ouko ateuliwa kumrithi Ojwang’ katika Mahakama ya Juu

Obado ampiga Raila ‘knockout’ bunge la kaunti