• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Uholanzi yapepeta Gibraltar bila huruma katika gozi la kufuzu Kombe la Dunia

Uholanzi yapepeta Gibraltar bila huruma katika gozi la kufuzu Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

UHOLANZI walimiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha pili cha mechi dhidi ya Gibraltar na kusajili ushindi wa 7-0 katika pambano hilo la kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Steven Berghuis alifungia Uholanzi bao la kwanza katika dakika ya 41 kabla ya Memphis Depay anayechezea Olympique Lyon ya Ufaransa kucheka na nyavu mara mbili.

Magoli mengine ya Uholanzi yalitiwa kimiani kupitia Luuk de Jong, Georginio Wijnaldum, Donyell Malen na Donny van de Beek.

Matokeo hayo yalisaza Uholanzi wanaonolewa na kocha  Frank de Boer katika nafasi ya pili kwenye Kundi G kwa alama moja nyuma ya Uturuki.

Kabla ya mechi hiyo dhidi ya Gibraltar, De Boer alikuwa amefichua kwamba maazimio yao masogora wake yalikuwa ni kusajili ushindi wa angalau mabao matano.

Hata hivyo, mabao yao yalikawia sana licha ya kujivunia umiliki wa mpira kwa asilimia 82 na kuelekeza makombora 19 langoni mwa wenyeji wao.

Kipa Dayle Coleing wa Gibraltar anayechezea kikosi cha Glentoran cha Ligi Kuu ya Ireland, alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Depay, Berghuis na kiungo wa zamani wa Everton, Davy Klaassen.

Beki wa zamani wa Manchester United, Daley Blind aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kupata jeraha baya la goti mwanzoni mwa kipindi cha pili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ubelgiji bila De Bruyne na Lukaku yakomoa Belarus 8-0

Ronaldo na Jota watambisha Ureno dhidi ya Luxembourg