• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Waathiriwa 800 wa mkasa wa moto na mafuriko  katika wodi ya landimawe wapokea msaada wa chakula kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi

Waathiriwa 800 wa mkasa wa moto na mafuriko katika wodi ya landimawe wapokea msaada wa chakula kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

WATU 800 kutoka mitaa ya mabanda mbalimbali katika wodi ya Landi Mawe, kaunti ndogo ya Starehe walioathirika na majanga tofauti walipokea msaada wa chakula jana kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.

Aidha, waathiriwa hao walishirikisha waliolazimika kuhama baada ya mafuriko kuvuruga makao yao mnamo mwezi wa Aprili mwaka huu.Vilevile, wengine walikuwa ni pamoja na waathiriwa wa mkasa wa visa viwili vya moto ambapo nyumba zao ziliteketea katika eneo la Kambi Moto sawia na eneo la Bundalangi mwezi huu.

Maeneo yote mawili yamo ndani ya mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba ulioko kwenye tarafa ya South B.Akiongea na Taifa Leo, mwakilishi wa wodi ya Landi Mawe, Bw Herman Kaimosi Azangu alisema msaada huo ulitoka kwa Hazina ya majanga ya kaunti ya Nairobi.

“Msaada huo wa chakula umetolewa na Kaimu Gavana wa Nairobi, Bi Anne Kananu kuwafaa wakazi walioathiriwa na majanga katika maeneo ya Mukuru kwenye wodi ya Landi Mawe,” Bw Azangu akanena.Mwanasiasa huyo alikariri kwamba msaada huo wa chakula ulikuwa ni pamoja na unga wa mahindi, mchele pamoja na sukari.

Fauka ya hayo, aliongeza kwamba walioathirika wameumia kwa muda wakiomba usingizi baada ya nyumba zao kusombwa na maji huku mali yao ikiharibiwa na maji.Kando na nyumba kuvurugwa na maji, wenzao walibakia bila kitu baada ya nyumba zao kuteketea kwenye visa vya moto na kuwaacha maskini hoehae na kubakia wakianza maisha upya.

Picha/SAMMY KIMATU
Herman Azangu Kaimosi

 

“Moto uliteketeza mali pamoja na yumba zao. Watoto wao hawakusazwa na ndimi za moto huku vitabu na sare za shule za wanafunzi zikiteketea na kuwa majivu,” Bw Azangu asema.Kadhalika, aliongeza kwamba katika kutoa msaada huo, wengine waliopatiwa chakula ni familia mayatima, wagonjwa wa virusi vya ukimwi, wakongwe sambamba na walemavu.

“Kwenye orodha ya mheshimiwa gavana, Bi Anne Kananu, aliwahesabu ndani wazee, mayatima, wagonjwa wa virusi vya ukimwi, walemavu na baadhi ya waliofutwa kazi kufuatia kuripotiwa kwa janga la Corona.

Hafla hiyo ilifanyika kwenye ofisi za mbunge wa kaunti zilizoko katika mtaa wa mabanda wa Commercial.Ili kujiepusha na hafla hiyo kuvurugwa na vijana wanaopenda kuzua balaa na rabsha, siku hizi, Bw Azangu alibuni mbinu mpya za kupeana misaada.

“Baada ya kujifunza na hafla zingine za hapo awali ambapo vijana walikuwa wanazua zogo tukipeana chakula kwa kuwanyang’anya akinamama tulivyowapatia, saa hii huwaita waathiriwa ofisini kwa awamu na tena siku mbalimbali lakini wakiwa kwa makundi mandogo tunapokumbatia kanuni za wizara ya afya dhidi ya kujikinga na msambao wa virusi vya Corona,” Bw Azangu akadokeza.

Picha/SAMMY KIMATU

  • Tags

You can share this post!

Hakimu aamuru muuzaji pombe kali akamatwe

Majumba ya kifahari yalivyogeuka maficho ya uhalifu utalii...