• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Watolewa hospitalini na kuuawa na umati

Watolewa hospitalini na kuuawa na umati

Na STEPHEN MUNYIRI

WANABODABODA wenye ghadhabu mnamo Alhamisi walivamia hospitali ya Karatina Level Four katika Kaunti ya Nyeri, wakawachukua kwa nguvu washukiwa wawili wa wizi wa pikipiki na baadaye kuwachoma.

Bodaboda hao walifanikiwa kuwachukua washukiwa baada ya kuwashinda nguvu polisi ambao walikuwa wakiwalinda.

Kinaya ni kuwa, wawili hao walikuwa miongoni mwa washukiwa wanne ambao awali walikuwa wameokolewa na polisi dhidi ya kuchomwa moto na umati, uliowatuhumu kuwa sehemu ya genge hatari katika kaunti ndogo za Mathira Magharibi na Mashariki.

Genge hilo linadaiwa kuendesha mauaji ya wahudumu wa bodaboda katika maeneo hayo na kuwanyang’anya pikipiki zao.

Mmoja wa washukiwa ambaye alikuwa amenaswa na bodaboda hao alinusurika kuchomwa na sasa amelazwa hospitalini akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Kundi moja la kutetea maslahi ya bodaboda eneo hilo lilikuwa limeeleza wasiwasi wake kufuatia ongezeko la visa vya mauaji ya wahudumu na kisha pikipiki zao kuibwa.

Mauaji hayo yalidaiwa kutekelezwa na wezi wanaojifanya wateja.

Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda cha Mathira, Bw Benjamin Mwangi, aliwataja baadhi ya wenzao waliouawa kama Timothy Wanjohi, Elisha Wahogo, William Kirii, Ian Wanjohi na Eliud Wambu, aliyeuawa majuzi. Alisema wana wanachama zaidi ya 3,000.

Purukushani ilizuka katika hospitali hiyo mamia ya wahudumu walipoingia na kuwashinda nguvu walinzi pamoja na polisi waliokuwa wakiwalinda washukiwa.

Baada ya kuwapiga, wahudumu walichoma miili ya washukiwa nje ya lango kuu la hospitali hiyo huku polisi wakitazama wasijue la kufanya.

Hali ya taharuki ilitanda mjini Karatina jioni hiyo polisi walipoanza kuwatawanya bodaboda hao.

Maafisa walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya, kwenye operesheni iliyoongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mathira Mashariki, Bw James Barasa.

Kisa hicho kinajiri huku mauaji ya wanabodaboda yakiendelea kushuhudiwa katika eneo hilo katika muda wa miezi mitatu iliyopita. Kufikia sasa bodaboda sita wameuawa katika hali tatanishi.

Alhamisi, tandabelua ilianza baada ya wahudumu kuwakamata washukiwa watatu na kuanza kuwapiga.

Baadaye, walienda kwenye makazi ya washukiwa kijijini Ndaro-ini wakachoma nyumba zao.

Kisha wakaelekea hospitalini ambako washukiwa walikuwa wamelazwa na kuwatoa kwa nguvu

Waliwavuta hadi nje ya lango kuu wakawapiga na kuwachoma.

Bw Barasa alisema polisi walizidiwa nguvu na umati huo, hivyo hakuna lolote ambalo wangefanya kuzuia mauaji hayo.

“Ni kweli polisi wetu walizidiwa nguvu lakini tuliitisha usaidizi. Wawili hao walitolewa hospitalini kwa nguvu na kuuawa na wahudumu hao. Hata hivyo, tulifanikiwa kumwokoa mmoja wa washukiwa,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Watanzania waulizia aliko rais huku serikali ikinyamaza

TAHARIRI: Klabu za ‘kikabila’ zitastawisha soka