• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Wezi wajipikia ugali, nyama na kushukuru familia kwa ushirikiano

Wezi wajipikia ugali, nyama na kushukuru familia kwa ushirikiano

WYCLIFFE NYABERI na RICHARD MUNGUTI

POLISI mjini Nyamira wanawasaka wahalifu wa kuthubutu kupitiliza ambao waliingia kwenye boma moja, wakajipikia ugali kwa nyama kisha wakashuruku familia hiyo walipokuwa wakitoroka na mali waliyoiba.

Kulingana na ripoti ya polisi, kisa hicho kilitokea Jumanne usiku kijijini Bomondo, ambapo majambazi hao walimvamia Bw Stephen Gichana alipokuwa akisubiri katika lango la nyumba yake afunguliwe wakati genge la watu wanane waliovalia jaketi sawia na zile za polisi lilipomvamia na kumpiga utosini kwa kifaa butu, na kumlazimisha amwamuru mwanawe afungue geti hilo.

Wahalifu hao walipoingia ndani ya nyumba waliwafunga kwa kamba Bw Gichana, mkewe na mwanao.

Kisha walisaka kote chumbani na kuchukua bidhaa muhimu kabla ya kufululuza hadi jikoni na kuchukua nyama iliyokuwa kwenye friji, wakaipika na kuila kwa sima waliyoisonga.

Baada ya masaa mawili chumbani humo, wezi hao waliwashukuru jamaa hao kwa ushirikiano wao mwema kabla ya kuondoka na kutokomea kusikojulikana.

Polisi wanaendelea na msako dhidi ya wahalifu hao.

Mtoto akataa mama yake

Kwingineko, kizaazaa kilitokea Jumatano katika mahakama moja ya Nairobi mtoto mvulana alipokataa kuandamana na mama yake mzazi kama korti ilivyokuwa imeamua.

Mvulana huyo alikaidi agizo la hakimu anayesikiza kesi za mizozo ya watoto kwamba awe akiishi na kutunzwa na mama yake, lakini mvulana huyo alikataa kata kata kuandamana na mama yake peupe.

Mama huyo alikuwa amewasilisha kesi mahakamani akiomba apewe idhini ya kuishi na kumlea mvulana huyo mwenye umri wa miaka 10.

Baada ya uamuzi wa korti, mvulana huyo alichomoka mbio huku akifuatwa unyonyo na mama yake lakini akamshinda kasi, akajiunga na baba yake na kumkwamilia.

Mama yake alijaribu kumfuata lakini mtoto akapiga duru. Wakili wa mwanamke huyo alijaribu kumshika mtoto huyo amkabidhi mama yake lakini ikawa ni kazi bure.

Ilibidi warudi mbele ya mahakama ya kuamua kesi za watoto kupata maagizo mengine kwa vile mvulana alikaidi agizo la hakimu.

You can share this post!

Gor Mahia waaga CAF Champions League baada ya kupokezwa...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 271 idadi jumla...