• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:59 AM
Wito Azimio waachane na maandamano watoto wasome

Wito Azimio waachane na maandamano watoto wasome

NA LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya nchi kuwa na amani ili wanafunzi wasome wakiwa kwenye mazingira mazuri, wamesema viongozi.

Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro ametoa wito kwa upinzani usitishe mipango yake ya maandamano ili wanafunzi wapate mazingira mazuri ya masomo.

“Tunawataka wapinzani wetu waipatie serikali ya Kenya Kwanza muda wa kufanya maendeleo badala ya kuzua taharuki hapa nchini,” alisema Bw Nyoro akiwa mjini Thika mnamo Jumamosi.

Kiongozi huyo alikuwa mgeni wa heshima katika hafla ya kupeana zawadi kwa shule za msingi na za upili zilizofanya vizuri masomoni.

Katika hafla hiyo shule za msingi zilizoorodheshwa kufanya vizuri masomoni ni Gatumaini, Queen of Rosary, na PrimeRose Academy.

Kwa upande wa shule za upili, zilizotia fora ni Maryhill Girls, Chania High, na Thika High.

Shule hizo zote zilitunukiwa vikombe.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a aliwarai viongozi wa upinzani kutoa nafasi kwa Rais William Ruto kutekeleza wajibu wake.

“Upinzani ufanye jambo la busara kwa kumpa nafasi kiongozi wa nchi atimize ahadi alizotoa kwa Wakenya,” alisema mbunge huyo.

Alisema ni vyema wanafunzi wapewe nafasi ya kujiendeleza kimasomo bila kutatizwa na yeyote.

“Tunajua maandamano yatavuruga masomo nchini na kwa hivyo hayana maana yoyote,” alisema Bi Ng’ang’a.

Mwalimu mkuu wa Chania High Bw James Gitau alisema shule yake inahitaji mabweni zaidi baada ya kupata idadi kubwa ya wanafunzi.

“Tuna idadi kubwa ya wanafunzi na inatulazimu kutumia mahema huku ujenzi wa mabweni kadha ukiendelea,” alisema kinara huyo wa Chania.

Alisema wakati huu wanafunzi wanahitaji mazingira mazuri ya elimu ili wafanye mitihani yao kwa utulivu.

Naye mwalimu mkuu wa Thika High Bw Julius Muraya alisema shule yake ina idadi kubwa ya wanafunzi lakini wanajizatiti kuona ya kwamba wanawapa elimu kwa njia inayofaa.

“Sisi walimu haja yetu ni kuona kila mwanafunzi anafanya vyema masomoni,” alifafanua Bw Muraya.

Mkurugenzi wa elimu kaunti ndogo ya Thika Magharibi Bw Maurice Sifuna alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba shule zote zinatendewa haki kielimu.

“Wakuu wote wa shule wanastahili kuhakikisha kuwa shule zao zinadumisha nidhamu na kufuata sheria zote za masuala ya elimu nchini,” alisema Bw Sifuna.

  • Tags

You can share this post!

Mtoto Sagini: Washtakiwa waliomng’oa macho wasukumwa jela...

Azimio kuwasha mishumaa kesho Jumatano

T L