• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Azimio kuwasha mishumaa kesho Jumatano

Azimio kuwasha mishumaa kesho Jumatano

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya umetangaza kusitishwa kwa maandamano ya kupinga serikali yaliyoratibiwa kufanyika Jumatano kote nchini.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu jioni, muungano huo ulisema badala yake viongozi wake na wafuasi watafanyama maandamano na mkesha kwa heshima ya waathiriwa wa ukatili wa polisi sehemu mbalimbali nchini.

“Kwa hivyo, tunatoa wito kwa Wakenya kujitokeza na kuwasha mishumaa na kuweka maua, haswa yale meupe, kwa ukumbusho wa wenzetu waliouawa na polisi kinyama katika maandamano ya amani siku zilizopita,” taarifa hiyo ikasema kuwa “maandamano ya  Jumatano, Julai 26, 2023 yatakuwa tofauti.”

Azimio pia ilisema siku hiyo viongozi wake wataanzisha mpango wa kuzifikia familia za wahasiriwa wote kwa lengo la “kutoa aina zozote za misaada ambayo itawapunguzia mizigo”.

“Wakati wa ‘kesha, uwashaji wa mishumaa na uwekaji maua, tunatoa wito kwa Wakenya kufanya maombi na kutaja majina ya wahanga wote,” taarifa hiyo ikaongeza.

Orodha ya majina ya waliokufa na wale waliojeruhiwa itatolewa mapema kwa ajili ya shughuli hiyo, Azimio ikasema.

“Aidha, tunatoa wito kwa Wakenya kuomba ili Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) iweze kushughulikia suala hilo la ukatili wa polisi kwa misingi ya orodha pana ya wahusika ambayo tumewasilisha kwa mahakama hii,” ikasema.

Muungano huo unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ulisema kuwa kufikia sasa jumla ya watu 50 wamethibitishwa kuuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa kutokana na ukatili ambao polisi walitumia dhidi ya waandamanaji.

“Hospitali nyingi zimeagizwa kutotoa idadi ya watu waliokufa, waliolazwa au hata kuwahudumia watu waliofika huko kusaka huduma za matibabu. Hii ina maana kuwa watu wetu wanauguza majeraha majumbani mwao ilhali wengine wamekufa na vifo vyao kutoripotiwa,” Azimio ikaeleza.

Kwenye kikao na wanahabari Jumamosi, vinara wa Azimio wakiongozwa na Kalonzo Musyoka walitangaza kuwa maandamano yatarejelewa Jumatano wiki hii.

“Hata hivyo, maandamano hayo yatakuwa siku moja pekee, Jumatano Julai 26, 2023 kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni,” akasema Bw Musyoka ambaye pia ni kiongozi wa Wiper.

Azimio imeahirisha maandamano hayo saa chache baada ya Waziri wa Usalama Kithure Kindiki kuonya kuwa maafisa wa polisi watakabiliana na wandamanaji kwa nguvu tosha kwa mujibu wa sheria.

“Tutatuma polisi siku hiyo majira ya alfajiri ili kuzuia visa vya uporaji wa mali ya umma na uharibifu wa miundo msingi. Ningependa kuwahakikishia kuwa nguvu ambazo tulitumia katika maandamano ya siku tatu wiki jana zilikuwa kidogo. Nguvu ambazo tutatumia Jumatano zitakuwa zaidi,” Profesa Kindiki akasema alipozuru eneo la Kiseria, Baringo Kusini, kaunti ya Baringo kukagua hali ya usalama.

  • Tags

You can share this post!

Wito Azimio waachane na maandamano watoto wasome

Wazee wampongeza Uhuru kwa kusema ‘Ruto ni prezzo...

T L