• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Wito serikali ipige jeki sekta ya juakali

Wito serikali ipige jeki sekta ya juakali

Na LAWRENCE ONGARO

MBUNGE wa Thika Bw Patrick Wainaina anaiomba serikali kuthamini na kupiga jeki sekta ya juakali.

“Serikali inastahili kusitisha baadhi ya bidhaa zinazotoka nchi za kigeni ili watu wa juakali waweze kufaidika na kazi ya jasho lao,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi alipozuru eneo la shughuli za juakali mjini Thika ili kujionea kazi inayofanywa na mafundi waliopewa zabuni ya Sh1 milioni kuunda madawati ya shule katika mji wa Thika.

Alisema tayari madawati 126 yameundwa na yatasambazwa katika shule tofauti eneo la Thika na vitongoji vyake.

Aliwahimiza vijana popote walipo wajiunge pamoja ili waweze kupewa fedha za Uwezo Fund ili waendeshe biashara zao.

“Ninawashauri vijana wajiunge kwa makundi ya watu kumi halafu waseme wanataka biashara ipi ya kujiendeleza nayo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema iwapo serikali itakuwa na mpangilio maalum bila shaka vijana wengi watapata jambo la kufanya na tutapunguza uhalifu mitaani.

Alitoa pendekezo kwa serikali kupitisha sheria ambapo bidhaa zote zinazoingizwa nchini kutoka nje zinatozwa ushuru hata mara nne ili kuwapa walioko katika sekta ya juakali fursa ya kujiendeleza na biashara zao.

“Kwa sababu ya ugumu wa maisha kila mmoja anajaribu kwa vyovyote vile kuona ya kwamba anajitafutia riziki yake,” alifafanua mbunge huyo.

Mkazi Francis Kimani ambaye huunda masanduku ya mabati katika anaiomba serikali iwajali ili pia wao wafaidike.

“Tunapongeza jinsi ambavyo mbunge wetu anatujali lakini serikali inastahili kutujali zaidi,” alisema Kimani.

You can share this post!

ANC kusajili wanachama wapya

Faida za pilipili mboga