• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Inspekta wa polisi jambazi azuiliwa akijaribu kuiba katika duka la M-pesa

Inspekta wa polisi jambazi azuiliwa akijaribu kuiba katika duka la M-pesa

NA STEVE OTIENO

POLISI wa cheo cha Inspekta amegeuzwa mahabusu katika kituo cha polisi cha Ruiru, Kiambu, baada ya kukamatwa akijaribu kuibia mteja kwenye duka la M-pesa akitumia bastola.

Nahason Ekidor alikamatwa na walinzi wa benki ya Equity mjini Ruiru, alipokuwa akitoroka umati wa watu waliojawa na hasira.

Kwenye tukio hilo la Jumamosi asubuhi, mwanaume aliyetambuliwa kama Peter Kimani ambaye pia anamiliki duka la M-pesa, alikuwa ameenda kuweka Sh200,000 kwa duka la M-pesa linalohudumiwa na Bi Mary Anne Njoki.

Ripoti za polisi zinasema punde tu Bw Kimani alipofika kwenye duka la M-pesa, mwanaume aliyekuwa na bastola aliingia humo na kumwamuru ampe pesa alizokuwa akiweka.

Bw Kimani aliambia Taifa Leo kwamba alikuwa tayari amempokeza Bi Njoki pesa hizo. Kwa kuwa alikuwa karibu na mlango wa duka hilo, alitoka nje mbio na kuanza kupiga mayowe. Naye Bi Njoki alipiga nduru kutaka usaidizi zaidi, kwa kuwa alikuwa amechwa ndani ya duka lake pamoja na mwanaume huyo mwenye silaha.

Umati uliitikia wito wa kelele na kuanza kufika sukani hapo. Alipogundua kuwa hakuwa na uwezo wa kukabiliana na umati uliokuwa unazidi kuongezeka, mwanaume huyo alifyatua risasi hewani na kuamua kutorokea usalama wake kwenye benki ya Equity.

Hapo, walinzi kwenye benki walimkamata na kumpokonya bastola hiyo. Koplo Thomas Mungai aliiwasilisha bastola hiyo kwa Kamanda wa DCI katika kituo cha polisi cha Ruiru.

Polisi waliokuwa karibu na eneo la tukio walimchukua Bw Ekidor na kumfungia seli, huku umati ukomba nafasi umfunze adabu.

Uchunguzi wa awali ulithibitisha kuwa Ekidor ni afisa wa polisi wa kitengo cha Recce cha Ruiru. Kitengo hicho kuwa na maafisa wa polisi wanaohusika na usalama wa watu mashuhuri, hasa Rais na naibu wake.

Bastola yake aina ya glock ambayo kawaida hubeba risasi 15, ilikuwa na risasi 14.

Polisi pia walifanikiwa kupata Sh54,100, huku wakiendeleza uchunguzi wa kisa hicho.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Makaburi mapya yafichuka Shakahola na kurudisha darubini...

Familia yahangaikia Sh300,000 kurejesha mwili wa jamaa...

T L