• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Tarajia DCI mlangoni pako iwapo umejiunganishia stima bila idhini ya Kenya Power

Tarajia DCI mlangoni pako iwapo umejiunganishia stima bila idhini ya Kenya Power

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power sasa inashirikiana na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika mpango wake wa kuzima uharibifu na wizi wa mitambo yake kuzuia visa vya kupotea kwa kawi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Joseph Siror amesema kuwa DCI imewatuma maafisa wake 42 kushirikiana na maafisa wa kampuni hiyo kuzima wizi wa nyaya za stima, uharifu wa transfoma na kuwafurusha watu waliojenga vibanda sehemu za kupitishiwa nyaya za stima.

“Katika mwaka wa kifedha uliopita, kampuni hiyo iliandikisha ongezeko la visa vya uharibifu wa transfoma kwa kima cha asilimia 46 ambapo jumla ya transfoma 242 ziliharibiwa ikilinganishwa na 165 iliyoharibiwa mwaka uliotangulia. Visa kama hivi pamoja na wizi wa nyaya ndivyo huchangia stima kupotea na kuathiri wateja wetu,” Bw Siror akasema kwenye taarifa Alhamisi, Novemba 16, 2023.

“Hii ndio maana kampuni hii sasa inashirikiana na asasi mbalimbali, ikiwemo DCI kupambana na maovu haya. Tunaamini ushirikiano huu na DCI utaimarisha uwezo wetu wa kuzima wizi wa mitambo yetu na maovu mengine kwa kukumbatia mfumo wa kijasusi,” Bw Siror akaongeza.

Alieleza kando na visa hivyo kuchangia Kenya Power kupata hasara, uharibifu wa transfoma na wizi wa stima unaweka hatarini maisha ya wananchi.

“Vile vile, maovu haya yanaathiri pakubwa ukuaji wa kiuchumi kwa sababu kawi ni hitaji kubwa katika ufanikishaji wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa,” Bw Siror akasema.

Kulingana na afisa huyo, tangu Julai mwaka jana, jumla ya watu 1, 026 wamekamatwa sehemu mbalimbali nchini kwa kuhusika katika uvurugaji wa mtandao wa usambazaji umeme.

Watu 472 miongoni mwao walikuwa ni washukiwa wa uharibifu wa transfoma na mitambo mingine ya Kenya Power.

Bw Siror aliongeza kuwa watu 320 wamekamatwa kwa tuhuma za wizi wa stima huku 33 walikitiwa mbaroni kwa kujenga vibanda katika maeneo yaliyotengewa kupitishiwa nyaya za stima.

Jumamosi wiki jana, stima zilipotea sehemu nyingi nchini, tukio ambalo Kenya Power ilisema lilichangiwa na hitilafu katika kituo chake cha Olkaria.

Kilikuwa ni kisa cha tano cha stima kupotea kote nchini ndani ya miaka mitatu. Mnamo Agosti 20, mwaka huu stima zilipotea kote nchini kwa zaidi ya saa 20, hali iliyochangia wateja kupata hasara kubwa.

  • Tags

You can share this post!

Bunge lakaidi mahakama na kuidhinisha polisi 1,000 watumwe...

Seneta wa zamani katika kesi ya ulaghai wa gari adai...

T L