• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
AU yakashifu ghasia Afrika Kusini, watu 72 wakiuawa

AU yakashifu ghasia Afrika Kusini, watu 72 wakiuawa

Na MASHIRIKA

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

UMOJA wa Afrika (AU) Jumatano ulikashifu vikali ghasia zinazoendelea kushuhudiwa nchini Afrika Kusini, huku ukitoa wito kwa mzozo huo kutafutiwa suluhisho la haraka.

Kufikia Jumatano, watu 72 walikuwa wamethibitishwa kufariki kutokana na ghasia hizo.

Mwenyekiti wa tume ya muungano huo, Moussa Faki Mahamat, alionya kuwa huenda ghasia zikasambaa katika nchi jirani ikiwa hali hiyo haitasuluhishwa.

“Ni lazima hali ya dharura irejeshwe ili kudhibiti ghasia hizo dhidi ya kuenea katika maeneo mengine. Kuna haja raia kuzingatia kanuni za kisheria,” akasema mwenyekiti huyo kwenye taarifa.

Kufikia Jumatano, ghasia hizo zilikuwa zimedumu kwa siku tano mtawalia. Waandamanaji wanalalamikia hatua ya serikali kumfunga gerezani aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jacob Zuma.

Mamia ya maduka yamevunjwa na kuporwa na baadhi ya makundi ya uhalifu yanayodaiwa kuwa miongoni mwa waandamanaji hao.

Wenyeji pia wamechukua hatua hiyo kulalamikia pengo kubwa la kimapato ambalo limekuwepo kwa miaka 27 tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru.

Kulingana na taarifa za polisi, zaidi ya watu 1,200 wamekamatwa katika mikoa ya Gauteng na KwaZulu-Natal, ambayo ndiyo imekumbwa na ghasia hizo kwa kiwango kikubwa.

Mnamo Jumanne, waandamanaji wenye ghadhabu walivamia kituo kimoja cha redio na kufanya uporaji.

Kutokana na ghasia hizo, baadhi ya vituo vya kutoa chanjo dhidi ya virusi vya corona vilifungwa baada ya shughuli hizo kuvurugwa.

Hatua ya serikali kutuma zaidi ya wanajeshi 2,500 kuwasaidia polisi kukabiliana na uporaji huo hazijafaulu.

Jumatano, polisi walisema ghasia hizo zishasambaa katika mikoa ya Mpumalanga na Northern Cape.

Mwanahabari wa shirika la AFP alisema aliona duka kadhaa zikiporwa katika mji wa Hammersdale, mkoani Mpumalanga.

Vituo vya televisheni vilionyesha uporaji zaidi ukiendelea katika miji ya Soweto na Durban.

Polisi wamesema watawakabili vikali wale ambao watapatikana wakipora mali ya wenyewe au wakiharibu mali.

Kituo cha mafuta cha Sapref kilicho jijini Durban pia kilifungwa kwa muda. Kituo hicho ndicho kikubwa zaidi nchini humo.

Kituo hicho hutoa zaidi ya mapipa 180,000 ya mafuta kwa siku.

Mfanyabiashara Tumelo Mosethli, anayehudumu jijini Johannesburg, alisema kuwa itakuwa vigumu kurejesha ajira zilizopotea kutokana na hali mbaya ya uchumi wa taifa hilo.

“Ni hali ya kutamausha sana kuona maduka na biashara za watu zikiporwa,” akasema.

“Ni kweli, watu wana njaa leo, lakini hali ya ukosefu wa ajira itaongezeka zaidi. Ni hali itakayoleta mahangaiko mengi katika nchi inayojaribu kuimarisha uchumi wake tena kutokana na athari za janga la virusi vya corona,” akaongeza.

You can share this post!

Je, IEBC yafaa kuanza kujiandaa kwa kura ya maamuzi kabla...

IEBC imeainisha wazi mazingira ya kituo cha kura –...