• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
AKILIMALI: Kilimo cha pilipili chabadilisha maisha ya wakazi Kilifi

AKILIMALI: Kilimo cha pilipili chabadilisha maisha ya wakazi Kilifi

Na MAUREEN ONGALA

MAENEO ya Magarini, Ganze na Kaloleni ni miongoni mwa yaliyo kame zaidi katika Kaunti ya Kilifi na ambayo yanazidi kuathirika kwa ukosefu wa mvua ya kutosha kufanyia kilimo cha vyakula aina nyingi.

Kwa miaka mingi sasa, wakulima katika maeneo hayo wamepata hasara kutokana na upanzi wa mahindi wakifuata desturi ya jamii nyingi nchini.

Wakazi hao wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada kutoka kwa wakulima wa kaunti za nje na wahisani.

Hata hivyo, kuna baadhi yao ambao wameamua kutumia mvua kidogo inayopatikana kukuza pilipili huku pia wakilazimika mara kwa mara kunyunyizia mimea yao maji.

Kilimo cha pilipili aina ya Kachachawa, imekuwa suluhisho kwa changamoto ya njaa na umaskini unaosababishwa na ukosefu wa pesa.

Wakulima hawa wametoka katika dimbwi la umaskini na kwa sasa wanafurahia matunda ya ukulima huo, wengi wao wakieleza kuwa wamefaulu kujenga nyumba nzuri, kununua mifugo na pia kuwapeleka watoto wao shuleni.

Ni safari ndefu kupitia milima na mabonde kuelekea katika kijiji cha Balagha kilicho eneo bunge la Magarini hadi katika shamba la Nyevu Nyawa.

Tulimkuta Nyevu akiwa katika shamba lake lililo karibu na kingo ya mto wa Galana akiendelea kunyunyuzia mimea ya pilipili maji.

“Nashukuru sana mmea wangu wa pilipili kwa sababu sikosi pesa. Wajukuu wangu hawalali njaa na pia nilinunua mbuzi ambaye amezaa watoto watano kwa sasa,” anasema Nyevu.

Anaeleza kuwa mnamo 2015, alipata hasara kubwa baada ya mimea yake kusombwa na maji baada ya mto Galana kufurika.

Hali hiyo anasema ilimvunja moyo kwani hangeweza kupata pesa za kukimu mahitaji yake na alikuwa tayari amejitahidi kutafuta soko la zao lake la pilipili.

Baada ya mafuriko, maafisa wa kilimo kutoka kampuni ya Equator Kenya walimtembelea na kumhimiza kufufua kilimo cha pilipili. Kampuni hiyo ndiyo husaidia wakulima wadogo kupata soko la mazao yao ikiwemo nje ya nchi.

Maafisa hao walimpa mwelekeo na ushauri wa jinsi ya kukuza pilipili kutumia mbinu za kilimo za kisasa kwa lengo la kupata faida.

“Niliamua kupanda pilipili kwa sababu haiathiriki na ukame na pia ina faida nyingi. Tumejaribu kupanda mahindi lakini kila mwaka yananyauka kwa ukosefu wa mvua ya kutosha,” anasema.

Anaeleza kuwa ukosefu wa chakula kutoka shambani na wakazi kukosa pesa za kununua chakula kwa sababu ya umaskini kumewafanya kutegemea chakula cha msaada kutoka kwa serikali ya kaunti, ile ya kitaifa na wahisani kwa miaka mingi sasa.

Nyawa anasema kuwa alitumia faida yake kujenga nyumba ya mawe na kununua mbuzi wa maziwa. Nyanya huyo hutumia pesa hizo pia kununua chakula na pia kuwalipia wajukuu wake karo.

“Hapo mwanzo nilikuwa nikipata Sh8,000 kila mara ninapovuna na kuuza pilipili kabla ya mafuriko. Lakini sasa nina matumaini kuwa nitaanza kupata pesa nyingi kwa sababu ninapata ushauri wa kutosha kutokea wakati ninapopanda pilipili na pia sitahangaika kutafuta soko,” anasema.

Hata hivyo, anasema kuwa yeye hukodisha mashine ya kupiga maji kutoka mto Galana hadi shambani mwake kila mara anapotaka kunyunyizia mimea yake maji kwa Sh500.

Shamba lake limeunganishwa na mipira ya kusambaza maji kutoka Mto Galana.

Katika kipande kingine cha shamba, Nyawa alikuwa anaendelea kukausha pilipili ili kutengeneza mbegu.

Katika kijiji cha Nyamalasinene kilicho eneo la Adu/Kamale, kuna boma la Mzee Birya Kahindi, ambaye alianza kilimo cha pilipili miaka minane iliyopita.

Mzee Kahindi amekuwa akizunguka vijijini akiwahimiza wakazi kupanda pipili ili kuinua hali ya maisha yao.

“Nilipanda mahindi kwa muda mrefu lakini sikuwa ninapata chakula cha kutosha familia yangu na pia mazao hayakuwa yanatosha kuuza ili nipate karo ya watoto wangu. Hapo ndipo nilifanya uamuzi wa kuanza kupanda pilipili,”anasema.

Mzee Kahindi anakuza pilipili katika shamba la ekari mbili.

Anasimulia kuwa ilikuwa changamato kwa wakulima katika maeneo hayo wakati wa mwanzo kwani walikuwa wanalazimika kusafiri kwa mwendo mrefu kutoka Adu/Kamale hadi mjini Malindi ili kuuza mazao yao ya pilipili.

Wakulima hao walipata afueni baada ya kampuni hiyo ya Equator Kenya kufungua kituo cha kukusanya zao hilo kutoka kwa wakulima katika soko la Ramada.

“Kufunguliwa kwa kituo cha Ramada ilikuwa afueni kwetu lakini kuna baadhi ya wakulima ambao walivunjika moyo kufuatia changamoto za usafiri na wakawa wameamua kuacha ukulima wa pilipili,” anasema akieleza kuwa hali hiyo ilichangiwa na kucheleweshwa kwa malipo yao.

“Tulikuwa tumesalia wakulima wachache na ilitubidi kusafiri hadi Ramada kupeleka mazao yetu kwa sababu kampuni hiyo haingeweza kuharibu raslimali zake kuja kuchukua pilipili kutoka kwa wakulima wachache,” anaeleza.

Anaongeza, “Niliendelea kuwahimiza wakulima kuendelea kupanda pilipli kwa wingi ili kampuni iweze kufungua kituo cha kukusanya mazao yetu karibu.”

Kulingana na Mzee Kahindi, waliendelea kujikaza na kwa sasa kampuni ya Equator Kenya hukusanya zaidi ya kilo 700 za pilipili kila siku kutoka kwa wakulima hao.

Alipokuwa fukara, aking’ang’ana na kilimo cha pilipili huku akikosa pesa kwa sababu ya malipo yao kucheleweshwa, jamii ilimbandika jina la ‘Kahindi Boya’ kwani kila siku alionekana kutembea kwa mwendo mrefu akiwa amebeba mitungi mwili midogo ya maji ya kunyunyizia mimea yake.

Anasema kuwa kwa sasa anajulikana kama ‘Kahindi Pesa’ kutokana na utajiri wake aliovuna kwa kilimo cha pilipili.

“Jamii ilinikejeli kwani ilikuwa si jambo la kawaida kwa mwanamme kubeba maji kutoka kwenye bwawa ili kunyunyizia mimea lakini wameona matunda ya bidii zangu na umuhimu wa pilipili na wananiheshimu,” anaeleza.

Mzee Kahindi huvuna zaidi ya kilo mia moja za pilipili kutoka ekari moja ya shamba na huuza Sh60 kwa kilo moja.

Alitumia sehemu ya pesa aliyopata kujenga nyumba. Aliwahimiza hata wakazawana wake kupanda pilipili ili kuishi maisha bora.

Mkazamwanae, Eunice Kazungu huotesha miche ya pilipili ili kuwauzia wakulima wengine.

Eunice alianza ukulima wa pilipili mwaka wa 2016 na anauza kila mche kwa Sh5.

“Nashukuru mmea wa pilipili kwani umeniwezesha kununua cherehani baada ya kuuza miche,” aasema.

Anaeleza kuwa amepanda pilipili katika robo ekari ya shamba lake na huvuna kilo 29 za pilipili kila msimu.

Hata hivyo, alitaja ukosefu wa maji kama changamoto kubwa inayowakumba wakulima walio katika maeneo kame.

Anasema wakazi hao hulazimika kutembea kwa zaidi ya saa moja na nusu kwenda kuteka maji katika bwawa.

“Maji hayo hayatoshi mimea na matumizi ya nyumbani kwa sababu ukienda mara moja unachoka kutokana na mwendo mrefu na jua kali, na ukifika nyumbani hauna nguvu tena” anaeleza.

Lakini anasema kuwa kwa wakazi wenye uwezo, huwalipa bodaboda Sh250 kuwaletea mitungi mitano ya lita 20 ya maji kutoka kwenye bwawa hilo.

Eunice anahitaji mitungi kumi ya maji ili kutosheleza mahitaji yake ya ukulima na matumizi ya nyumbani na pilipili huvunwa kwa misimu miwili kila mwaka.

Katika kijiji cha Kipawa katika eneo bunge la Ganze ni nyumbani kwa Grace Shida.

Anasimulia kuwa alipoamua kuanza kilimo cha pilipili, alikumbana na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya jamaa zake.

Hata hivyo, hilo halikumvunja moyo kwani baada ya muda mfupi alianza kupata kiasi kikubwa cha fedha.

“Mara ya kwanza kuuza pilipili rafiki yangu aliniletea Sh4,000. Nilifurahi sana na kupata nguvu na moyo wa kuendeleza ukulima huo bila uoga,” anasema.

Anasema alipoelezea baadhi ya jamaa zake kuhusu pesa alizopata, hawakuamini na wengi walibadili mtazamo wao kuhusiana na kilimo hicho.

Shida anaeleza kuwa kiwango cha pesa zake kilizidi kuongezeka kila mara hasa baada ya mumewe kuanza kumsaidia katika kilimo hicho.

Alitumia pesa hizo kujenga nyumba na akanunua mbuzi wa kufuga wa maziwa.

Amepanda ekari mbili za pilipili na hupata Sh12,000 anapovuna.

Anasema kuwa mumewe pia amejiunga na klilimo hicho na kila mara wanapouza wao hukaa pamoja kupanga watakavyotumia pesa zao.

Wakulima wengi kutoka maeneo hayo wamekuwa wakiwezeshwa kuanzisha ukulima wa pilipili hiyo ya kachachawa kupitia mpango wa kustawisha kilimo unaofahamika kama Agricultural Sector Development Program (ASDP).

Ili kutatua changamoto kubwa ya ukosefu wa soko inayowakumba wakulima wengi wa mazao tofauti, wakuzaji pilipili wamepata soko kutoka katika kampuni ya Equator Kenya ambayo hununua mazao yao bila kuchelewa.

Mpango huo umewezesha Kaunti ya Kilifi sasa iwe na takriban wakulima 6,000 wa pilipili.

Bi Joyce Zawadi, 24, kutoka kijiji cha Vilakwe eneobunge la Ganze akiwa katika duka lake la kushona nguo kijijini Kachororoni huko Ganze. Alianza kupanda pilipili pamoja na mamake Bi Sidi Alfred baada ya kukosa karo ya kujiunga na shule ya upili mwaka wa 2016. Mapato ya kilimo cha pilipili yamemsaidia kujifunza ushonaji nguo mjini na kuanzisha biashara yake Kilifi. Picha/ Maureen Ongala

You can share this post!

KAMAU: Kuna ishara ghasia za 2007/08 zitatokea tena

Msimamo wa medali za Olimpiki 2020