• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
AKILIMALI: Matumizi ya vitunguu kukabili kero ya wadudu shambani

AKILIMALI: Matumizi ya vitunguu kukabili kero ya wadudu shambani

Na SAMMY WAWERU

WADUDU huwa kero ambazo hutatiza wakulima.

Ni kero inayojiri na gharama yake, hivyo basi kulemaza jitihada za wakulima waliokumbatia kilimo hasa kwa minajili ya biashara, kupiga jeki mapato na kujiendeleza kimaisha.

Huku wanazaraa wakihimizwa kudumisha kilimohai, kupitia mifumo asilia katika ukuzaji wa mimea, matumizi ya vitunguu ni kati ya wanayopaswa kutumia.

Maumbile ya vitunguu, hususan kwa sababu ya harufu yake huzuia wadudu waharibifu kwa mimea kukita kambi shambani.

“Vitunguu vikipandwa shambani, kandokando na kati ya mimea, hutimua wadudu,” anasema Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo.

Akihimiza wakulima kukumbatia mfumo wa vitunguu kukabili wadudu, mdau huyu anasema ni mojawapo ya njia bora kuafikia kigezo cha kilimo-hai au kilimo asilia.

Aidha, ni mfumo usiotumia dawa dhidi ya wadudu, ili kupata mazao salama. “Dawa za wadudu na magonjwa ya mimea haswa zenye kemikali huharibu udongo, kwa kuudhoofisha na kupunguza au hata kumaliza rutuba,” Mwenda anaonya.

Matumizi ya dawa na fatalaiza zenye kemikali, pia yanatajwa kuchangia magonjwa yanayohusishwa na lishe, kama vile Saratani.

Saratani pia Kansa ni ugonjwa hatari ambao unaendelea kusababisha maafa kwa waliugua.

Caroline Kinoti ni miongoni mwa wakulima waliokumbatia matumizi ya vitunguu kukabili wadudu.

 

Caroline Kinoti (kulia) ni mkulima wa matunda, akiwa shambani mwake eneo la Kirinyaga. Picha/ Sammy Kimatu

Ni mkulima wa mseto wa matunda, kuanzia karakara, ndizi, mapapai, kati ya mwa mengineyo, katika Kaunti ya Kirinyaga.

“Kwa kutumia vitunguu kukabili wadudu, gharama ya matumizi ya dawa katika mradi wangu wa matunda imepungua kwa kiasi kikuu,” asema mkulima huyu.

Aidha, amepanda vitunguu vya majani kandokando mwa shamba lake, na kati ya mimea anayokuza.

Charles Mwangi, mkulima wa mboga Nyeri, ambaye pia hutumia vitunguu kukabili shambulio la wadudu kwa mimea shmbani.

Hukuza spinachi, kabichi, brokoli, sukuma wiki na mboga tofauti za kienyeji. “Vitunguu ni ‘dawa’ murwa kufurusha wadudu shambani,” Mwangi aelezea, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo huo.

Ni muhimu kukumbusha kuwa vitunguu haviathiriwi na wadudu.

Yote tisa, vitunguu hivyo vinapokomaa, ni hela hatua ambayo inaongeza mapato kwa mkulima.

“Unaweza ukapanda vitunguu vya majani na vile vya viazi, vya mviringo (maarufu kama bulb onions. Vyote ni mapato kwa mkulima vinapokomaa,” mkulima Mwangi asema.

  • Tags

You can share this post!

Patrick Vieira apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa...

Bandari ya Lamu kuanza kutumiwa kuingiza mafuta ya nazi