• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Maguire alivyokataa kugwaya na kuibuka mnara imara wa Man United msimu huu

Maguire alivyokataa kugwaya na kuibuka mnara imara wa Man United msimu huu

 NA LABAAN SHABAAN

HARRY Maguire alikejeliwa na mashabiki wa upinzani na timu yake kwandama.

Akaishia kupokonywa unahodha. Ila, Maguire hakugwaya. Alisimama kidete akaweka kichwa juu na sasa yeye ni mnara katika ulinzi wa Manchester United.

Difenda huyu alicheka na nyavu mara mbili katika mechi mbili zilizopita.

Liverpool ilipochuana na United, alicheza kwenye safu ya mbele na kuzua hofu kwenye lango la the Reds.

Wakati walinzi wa United wamepata majeraha chungu taka, Maguire amebakia kuwa mhimili wa matumaini.

Licha hata ya Manchester United kudorora, fomu yake Maguire inafaa kusifiwa msimu huu.

Hakika, ni mmoja wa wachezaji waliojisabilia kisabuni ambao wanafaa kusazwa msimu ujao wakati United itafanya mageuzi uwanjani.

Sasa, mabingwa wa Uingereza mara 20 wametinga fainali ya kombe la FA na watakabana koo na Manchester City mnamo Mei 25.

Maguire alicheza kwa saa mbili kwenye mechi dhidi ya klabu ya daraja la pili Coventry katika mchuano wa nusu fainali akiwa na jeraha.

“Maguire alishiriki mchezo huo akiwa na jeraha kutoka mwanzo hadi mwisho,” alikiri kiungo mkabaji wa United Casemiro aliyetumiwa katika nafasi ya mlinzi wa kati

Mlinzi huyu alifunga bao katika mechi iliyoishia sare ya mabao matatu kabla ya kuamuliwa na mikwaju ya penalti.

Juma moja baadaye Maguire alitikisa kamba dhidi ya Sheffield United na kusaidia Red Devils kushinda 4 – 2.

Ni nadra sana mchezaji huyu kufunga goli ila kucheka na dimba mara mbili mfululizo ni tukio la kupigiwa mfano.

Maguire ambaye aliteuliwa na kocha aliyetimuliwa, Ole Gunnar Solskjaer, anafurahia msimu bora zaidi ukizingatiwa alivyoanza.

Alikuwa nusura auzwe kwenda West Ham kwa kima cha pauni 30 milioni kabla ya mshahara wake mnono kuwatisha ‘wananyundo’ hadi wakagwaya.

Difenda ambaye hakupendelewa miongoni mwa wenzake- Lisandro Martinez, Raphael Varane, Luke Shaw na Victor Lindelof – ameondokea kuwa tegemeo.

Amehiari kujasiri kukemewa na mashabiki baada ya kuboronga mchezoni katika misimu kadhaa.

Kama mfa maji, hakuchoka ila aliendelea kutapata hadi alipopata karata bora ya kumfanya kimbilio kwa kocha wake Erik ten Hag.

“Ili Maguire afane katika mechi, anafaa kustahimili kelele za mashabiki na kuendelea kucheza,” Ten Hag alisema awali.

Licha ya changamoto, Maguire amekuwa kwenye kikosi cha kwanza mara 24 msimu huu.

  • Tags

You can share this post!

Serikali ilifanya vizuri kutuondolea jukumu la nidhamu kwa...

Kindiki aamuru daktari gaidi atumikie kifungo cha miaka 12...

T L