• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Amabuko, Kaunti ya Kisii

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Amabuko, Kaunti ya Kisii

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili Amabuko (CHAKIA) kilianzishwa Oktoba 15, 2021 kwa lengo la kuboresha matokeo ya KCSE na kubadilisha mtazamo hasi wa baadhi ya wanafunzi kuhusu somo la Kiswahili.

Idadi kubwa ya wanafunzi sasa wamekuwa na ari ya kukichapukia Kiswahili tangu chama hiki kiasisiwe katika Shule ya Upili ya Amabuko iliyoko Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii.

Zaidi ya kuchochea maadili miongoni mwa wanafunzi, chama kimekuwa pia mstari wa mbele kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi katika sanaa mbalimbali kama vile uigizaji na uandishi wa kazi bunilizi.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Upili ya Amabuko, Kisii. PICHA | CHRIS ADUNGO

Laurine Mokua na Mourine Mobisa ambao ni wanafunzi wa kidato cha kwanza ni miongoni mwa wanachama ambao mashairi yao yamekuwa yakichapishwa katika gazeti la Taifa Leo na kupeperushwa hewani na idhaa mbalimbali za humu nchini kwenye vipindi vya lugha.

Hatua hiyo imewapa wanafunzi wengine motisha ya kujiunga na CHAKIA na kutunga mashairi kwa ghamidha. Chini ya uelekezi wa walezi wao, Mokua na Mobisa sasa wanaandaa diwani, ‘Karakana ya Ushairi’ itakayochapishwa hivi karibuni.

Chama pia kina kitengo cha uanahabari, ‘Zoom Complex Media’, kinacholenga kuwaamshia wanafunzi hamu ya kuwa wanahabari katika siku za usoni. Kinaongozwa na Daniel Mokaya, Wilson Okioyi, Lameck Omweri na Neuben Moruri ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu.

Kufikia sasa, CHAKIA kinajivunia wanachama 80 chini ya uongozi wa Emmanuel Nyang’au (kidato cha nne) na Millicent Marube (kidato cha tatu). Walezi wa chama ni Bw Duke Nyakundi, Bw Jared Nyamari, Bw Dominic Ondieki, Bi Jacinta Mwembi na Bw Fredrick Mayore.

 

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Nafasi ya Kiswahili na malengo ya Elimu...

FASIHI SIMULIZI: Fasili, sifa, dhima na aina za ngomezi

T L